SERIKALI ya Awamu ya Sita, kupitia kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeendelea kuhakikisha watoa huduma wazawa wananufaika na fursa zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia.
Hayo yamesemwa Mei 19, 2025 na Mkurugenzi wa PURA Mhandisi Charles Sangweni kwenye Mkutano na Wahariri na Waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mhandisi Sangweni alisema, kupitia usimamizi makini wa suala hili, ushiriki wa watanzania katika ajira umekuwa wa wastani wa asilimia 85 ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo ushiriki wa watanzania ulikua chini ya asilimia 50.
Alisema, manunuzi ya bidhaa na huduma za ndani imekuwa katika wastani wa asilimia 60 kwa bidhaa na huduma za ndani ikilinganishwa na asilimia chini ya 40 kwa miaka ya nyuma.
“Sambamba na hilo, PURA imeendelea kusajili watoa huduma wa kitanzania na watanzania waliosomea masuala ya mafuta na gesi asilia katika kanzi data ijulikanayo kama Common Qualification System (CQS),” alisema.
Aidha, Mhandisi Sangweni alisema, Serikali kupitia PURA itaendelea kuimarisha utendaji na usimamizi wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli ili kuhakikisha kuwa sekta ya nishati inaendelea kuchangia ipasavyo katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
“PURA itaendelea kushirikiana na wadau wakiwemo; sekta Binafsi ili kuimarisha upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuendelea kusimamia na kudhibiti shughuli ipasavyo shughuli za mkondo wa juu wa petroli,” alisema Mhandisi Sangweni.
Aliendelea kusema, tangu kupata uhuru Tanzania imepitia changamoto mbalimbali katika eneo la utafutaji wa mafuta na gesi, ambapo changamoto zilizojitokeza zilifanyiwa kazi na hatimaye kufikia hatua iliyopo sasa.
“Kumefanyika ugunduzi wa gesi asilia nyingi ambayo matumizi yake yana manufaa makubwa kwa Taifa haswa katika kuinua uchumi,” alisema Mhandisi Sangweni.
Aidha, Mkurugenzi huyo wa PURA aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mazungumzo ya utekelezaji wa mradi wa usindikaji wa gesi asilia kuwa katika hali ya kimiminika (yaani LNG project).
Alisema, mradi huo utaliletea Taifa manufaa makubwa kwa kuanzia fedha, ajira, uanzishwaji wa viwanda vinavyotumia gesi kama malighafi pamoja na uuzaji wa bidhaa mbalimbali.