Watanzania wanaoishi Brazil watakiwa kuzingatia sheria za nchi hiyo

0

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewasihi watanzania wanaoishi nchini Brazil kuzingatia sheria za nchi hiyo pamoja na kujihusisha na biashara halali katika nchi hiyo.

Makamu wa Rais amesema hayo alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Brazil uliopo Jijini Brasilia na kuzungumza na watumishi wa ubalozi huo ambapo alipokea taarifa ya baadhi ya watanzania kutumikia vifungo mbalimbali katika magereza nchini Brazil.

Amemsihi Balozi wa Tanzania nchini Brazil Dkt. John Simbachawene kufanya vikao na watanzania waishio Brazil kuwasisitiza kujielekeza zaidi katika fursa nzuri na zitakazotangaza vema Taifa la Tanzania.

Makamu wa Rais amewasihi kuhakikisha wanakuza diplomasia ya uchumi baina ya Tanzania na Brazil kwa kuwa Taifa hilo ni kubwa lenye idadi kubwa ya watu hivyo ina fursa ya masoko kwa bidhaa za Tanzania.

Pia, alisema nchi hiyo imewekeza vizuri katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, utafiti, viwanda pamoja, uchumi wa buluu pamoja na michezo hivyo ni fursa nzuri kushirikiana na Tanzania.

Amewataka kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini Tanzania pamoja na kuvutia wawekezaji. Pia amewaelekeza kuendelea kutafuta nafasi za masomo kwa watanzania ili waweze kunufaika na uwepo wa teknolojia mbalimbali zilizopo nchini Brazil.

Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa pili wa Brazil na Afrika kuhusu usalama wa chakula, mapambano dhidi ya njaa na maendeleo vijijini unaofanyika Jijini Brasilia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here