Wataalamu watakiwa kusimamia matumizi ya nishati safi ya kupikia

0

WATAALAMU wa mazingira katika mikoa yote nchini wametakiwa kuwa mfano na kuhamasisha na kusimamia matumzi ya nishati safi ya kupikia kwenye jamii.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Makamu wa Rais Sigsbert Kavishe wakati akifunga Kikao Kazi cha Wataalamu wa Mazingira Kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini ya Masuala ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini Aprili 12, 2025 jijini Dodoma.

Kikao hicho kilichofunguliwa Aprili 11, 2025 na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja, kimekwenda sanjari na zoezi la kukabidhi majiko sanifu yanayotumia nishati safi ya umeme kwa wataalamu wa mazingira wa mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Akifunga kikao kazi hicho, Kavishe alisema ni wakati sasa kwa wataalamu hao kushirikiana kwa pamoja na kufanyia kazi changamoto za kimazingira zilizoibuliwa na mikakati yake iliyowekwa vilete matokeo chanya katika nchi.

Kavishe aliwasisitiza wataalamu hao wa mazingira wa mikoa kuendeleza ushirikiano na maafisa viungo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi zao kwa ujumla ili kuhakikisha lengo la usimamizi wa mazingira linakuwa endelevu.

“Nina imani mtashirikiana katika kuhakikisha mnatoa elimu kwa wananchi kuhusu usafi wa mazingira, bustani za kijani, kutunza vyanzo vya maji, misitu, fursa zilizopo katika biashara ya kaboni, uchumi wa buluu na nishati safi,” alisema.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Mazingira Mkoa wa Mwanza Mangabe Mnilango alisema kikao hicho ni daraja kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na wataalamu wa mazingira wa mikoa hiyo, na hivyo kufanikisha kazi ya kuratibu masuala ya mazingira.

Aidha, alisema mkoa huo bado una changamoto ya magugu maji ambayo yameleta madhara katika sekta ya usafiri na mazingira. Katika kukabiliana nayo tayari Serikali imeanza kufanyia kazi changamoto hiyo.

Pia, Mnilango alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi katika mkoa wake kufuga kisasa kwa kutokuwa na mifugo mingi katika eneo moja kwani hali hiyo huharibu ardhi.

Naye Mtaalamu wa Mazingira wa Mkoa wa Mara Nawabi Miyola amewahamasisha wanawake na wananchi kwa ujumla kutumia nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama na muda katika mapishii.

Alisema, esema matumizi ya nishati safi ya kupikia husaidia wanawake kufanya majukumu mengine wakati wa kupikia badala ya kuzunguka kutafuta kuni kwenye misitu.

Vilevile, Nawabi ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwakabidhi majiko ya kisasa yanayotumia nishati safi ya umeme mdogo ambayo yatakuwa chachu kwao kuhamasisha wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here