Na Mwandishi Wetu
NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Prof. Tumaini Nagu amewataka wataalamu wa Dawa, Uchunguzi wa Afya na Mionzi pamoja na wadau wa mnyororo wa bidhaa za Afya kuandaa mpango kazi utakaowezesha kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya.
Prof.Nagu ametoa wito huo kwa wataalam hao katika ukumbi wa Dodoma Hoteli, wakati akifungua kikao kazi kilicholenga kupitia Mpango kazi wa usimamimizi wa bidhaa za afya na uchunguzi katika ngazi ya afya msingi.
“Andaeni mpango kazi utakaotekelezeka na kuendana na vipaumbele vya Taifa ili uboreshe upatikanaji wa bidhaa za afya, vifaa tiba, na huduma bora za uchunguzi wa afya kwa wananchi,” Prof. Nagu amesisitiza.
Sanjari na hilo, Prof. Nagu amehimiza kuwa, mpango kazi unaoandaliwa uendane Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 3-Afya Bora na Ustawi).
Prof. Nagu amewataka wataalamu hao kuandaa mpango kazi utakaokua ni dira ya usimamizi na utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa dawa, vitendanishi na huduma za uchunguzi kupitia radiolojia.
Prof. Nagu ameongeza kuwa, mpango kazi huo ulenge kuimarisha uzalishaji wa bidhaa hapa nchini ili kuboresha huduma za Dawa, vitendanishi na uchunguzi wa maabara na Radiolojia.
Aidha, Prof. Nagu amewataka wataalam hao kuzingatia eneo la uimarishaji wa mnyororo wa bidhaa za afya ili kuondoa upotevu wa bidhaa utokanao na kufa kwa dawa na vitendanishi.