MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Regina Bieda, amefungua kikao cha wataalam wa afya Mkoa wa Pwani kilicholenga kujadili vifo vitokanavyo na afya ya uzazi na watoto wachanga kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025 katika Mkoa wa Pwani.
Kikao hicho kimefanyika leo Mei 14, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kikihusisha wataalam wa afya kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Bieda alisema, maudhui ya kikao yanaonyesha uzito na umuhimu wake kwa wananchi, kwa kuwa suala la kuzuia vifo vya mama na mtoto ni nyeti na linagusa moja kwa moja ustawi wa jamii.
Aliongeza kuwa, kikao hicho kitakuwa msingi wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku kwa wataalam hao.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirye Wkio, alisema lengo la kikao hicho ni kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kuboresha utoaji wa huduma za afya katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma.
Naye Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Pwani, Happiness Ndelwa, ameeleza kuwa juhudi zilizofanyika zimezaa matunda ambapo vifo vya akina mama wajawazito vimepungua kutoka 16 katika robo ya pili (Oktoba hadi Januari) hadi kufikia vifo 9 katika robo ya tatu.
Aidha, vifo vya watoto wachanga (wenye umri wa siku 0 hadi 28) vimepungua kutoka 45 hadi 37 katika kipindi hicho, jambo linaloashiria hatua chanya katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.