Wasira: Watanzania kataeni kuyumbishwa na wasioitakia mema nchi

0

Na Mwandishi Wetu, Tabora

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Watanzania wasikubali kuyumbishwa na vyama vya siasa vyenye kuhatarisha amani na usalama wa nchi.

Amesisitiza kuwa amani iliyopo si mali ya chama cha siasa bali ni tunu ya Watanzania na lazima ilindwe.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira ameeleza hayo Aprili 15, 2025 alipokuwa akizungumza katika kikao cha ndani kilichowakutanisha viongozi wa Chama kutoka Wilaya ya Tabora Mjini na Uyui mkoani Tabora.

“Kuna vyama vya siasa ambavyo vinataka uhuru usiokuwa na mipaka, uhuru usiokuwa na amani hauna maana, na wako wanaotoka kulifanya suala hilo kama mtaji. Tunaposema nchi iko salama maana yake tuko salama kweli na wale wanaodhani tunaweza kutikiswa tunawapa majibu hawawezi kututikisa.

“Sisi Katiba yetu Ibara yake ya tano inasema CCM jukumu lake la msingi ni kushinda uchaguzi, kukamata dola, sasa lazima tukamate dola kwa sababu mapinduzi ambayo tunayaendesha kuleta maisha bora kwa watu hayawezi kupatikana bila sisi kushika dola.

“Kwa hiyo dola ni chombo chetu cha mapinduzi na hatuwezi kukikabidhi kwa chama kingine chombo hiki ambacho hakipo kwa ajili ya wenye vyama ambavyo tumesikia kule Njombe mwenezi aliletewa ‘longolongo’ alipigwa hadi mbavu zikavunjika, tena mwenezi wa kike, alichapwa na wanaume halafu chama cha namna hiyo mkipe dola mmechoka na amani?

“Amani unaweza kuizoea ukaona hata isipokuwepo wewe utakuwepo, haiwezekani, kajifunze kwa majirani zetu, ikitoweka hairudi. Nenda kaulize maeneo ambayo imetoweka hairudi hata kule ambako hali imetulia visasi vimebaki, visasi vinarithiwa vizazi kwa vizazi, msikubali mkababaishwa na jambo la msingi kuhusu amani yetu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here