Wasira atahadharisha wanaotumia mitandao kuleta chokochoko

0

Na Mwandishi Wetu, BUNDA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, ametoa tahadhari kwa wananchi dhidi ya kikundi cha watu wachache wanaoleta chokochoko katika mitandao ya kijamii.

Amesema kikundi hicho ni miongoni mwa watu wachache wasioridhika, hata hivyo kamwe hawatotimiza dhamira yao ovu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni za urais uliohutubiwa na Mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mjini Bunda, alisema amani na utulivu utaendelea kutawala nchini.

“Zipo chokochoko nyingi ambazo hazipo kwa watu, zipo kwa wacheche wanaotumia mitandao ya kijamii. Naomba msome ile mitandao kwa makini sana. Kuna watu hawaridhiki.

“Kinamama wanaopika maharage wanafahamu yapo maharage hata ukiyapika vipi yatatokea machache yakielea. Hayo hayaivi na ndiyo watu wanaosumbua,” alisisitiza.

Aliongeza: “Watu hao hawawezi kuisumbua nchi, namwambia mgombea wetu (Dkt. Samia) asibabaishwe na watu hao wachache, hata ukifanya vizuri namna gani wao wananuna, ndivyo walivyo.”

“Wapo watakaokumbuka kwa wema wenye nia njema. Dkt. Samia amefanyakazi kubwa, jinsi mnavyomuunga mkono hapa ndivyo anavyoungwa mkono Tanzania nzima,” alieleza.

Wasira alisema CCM imewaletea mgombea urais mwenye mafanikio makubwa ya utekelezaji ilani ya uchaguzi iliyopita na siyo mwenye uwezo mdogo.

“Hatuwaletei mgombea urais ‘lena’ tunawaletea mgombea urais aliye fanyakazi ya urais kwa mafanikio makubwa,” alisisitiza.

Alisema Dkt. Samia aliingia madarakani katika misukosuko mikubwa wakati ambao taifa lilikumbwa na ugonjwa wa Uviko-19, kufariki dunia kwa Rais aliyekuwa madarakani (Hayati Dkt. John Magufuli) na kushuka kwa uchumi.

Alieleza kuwa, Dkt. Samia alipoingia madarakani alitumia maneno mawili ambayo ni ‘Kazi Iendelee’.

“Alipewa mtihani mkubwa aliachiwa miradi mikubwa ya nchi yetu. Aliachiwa reli haijakamilika lakini leo imekamilika mpaka Makutupora ya Singida kilometa 722 kutoka Dar es Salaam.

“Aliachiwa bwawa la Mwalimu Nyerere lilikuwa chini ya asilmia 30, hata hivyo asilimia 70 imejengwa chini ya usimamizi wa Rais Samia na Tanzania ina umeme wa kutosha,” alibainisha.

Kwa upande wa elimu, Wasira alisema katika Wilaya ya Bunda Dkt. Samia amejenga shule mpya 13 za msingi, shule 15 za sekondari, zahanati 20, vituo vitatu vya afya na hospitali moja mpya.

Vilevile, alisema Dkt. Samia ametoa mchango mkubwa kupunguza vifo vya kinamama na watoto kwa kuwa alipoingia madarakani alikuta katika kila vizazi hai 100,000 vizazi 500 walifariki dunia kila mwaka.

Alieleza kuwa Dkt. Samia amewezesha kushusha hali hiyo ambapo sasa katika kila vizazi hai 100,000 mia tano walikuwa wakifarkki leo vimeshuka kufikia 100.

Awali, Mgombea Ubunge Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, alisema alipokabidhiwa Wizara ya Maji, alipewa maagizo na Dkt. Samia kuhakikisha hakuna mwanamke atakayeteseka kwa kukosa maji.

Alisema hali ya maji miaka minne iliyopita katika wilaya hiyo ilikuwa mbaya kwa kuwa miradi iligeuka kichaka cha watu kufanya ubadhirifu.

Aweso alisema Dkt. Samia alimwagiza kufika wilayani Bunda kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo huku akitoa sh. bilioni 10 kutekeleza mradi wa maji Nyabeho.

Alisema mradi huo umeshakamilika, wananchi wanapata maji safi na salama.

“Hapa tuna miradi mingi ambayo ipo ilikamilika na mengine ipo hatua mbalimbali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 20. Zaidi ya wananchi asilimia 87 eneo la Bunda Mjini wanapata huduma ya maji,” alieleza.

Alieleza kuwa maeneo yaliyokuwa na changamoto ya maji ni vijijini ambapo Dkt. Samia amechukua hatua kuhakikisha huduma hiyo inapatikana.

Waziri huyo alisema Dkt. Samia ametoa fedha zaidi ya Shilingi Bilioni 100 kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Bunda na Tarime.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here