Wasira amshangaa mbunge aliyesema anamdai Rais Samia

0

Na Mwandishi Wetu, Geita

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira, amesema amesikitishwa na mbunge (hamkumtaja jina) aliyesema anamdai Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wenzake hawana deni naye na kwamba mbunge huyo ameingia ‘choo’ ambacho sio chake.

Kauli ya Wasira inakuja siku moja tu baada ya Mbunge wa Jimbo la Kisesa mkoani Simiyu (CCM) Luhaga Mpina kuzungumza mbele ya Rais Dkt.Samia aliyekuwa ziarani mkoa humo kudai kwamba bado wanamdai Rais, hata hivyo Rais Samia alimwambia mbunge huyo anamshangaa kwa kusema bado anamdai.

Akizungumza na wanachama wa CCM katika kikao cha ndani kilichofanyika Juni 18, 2025 Geita Mjini, Makaku Mwenyekiti Wasira alisema amesikitishwa na rafiki yake mmoja (hakumtaja jina) kusema wanamdai Rais Dkt. Samia.

“Kwa hiyo nimesikitika rafiki yangu mmoja sitaki kumtaja jina yeye anasema sisi tunakudai anamwambia Rais. Wenzake wanasema miaka uliyokaa (Rais) umefanya mengi na hatuna deni na wewe hawakusema amemaliza matatizo yote,”

“Tunachosema kwa muda tuliokupa na kwa matatizo uliyotatua Rais unastahili kupewa muda zaidi kwa sababu umethibitisha kwamba unao uwezo mkubwa wa kusaidia nchi yetu.”

Akifafanua zaidi Wasira alisema, Rais amekaa madarakani na amefanya mengi lakini wako watu wanadhani unaweza kumaliza matatizo yote ndani ya miaka mitano, hao ni watu wa ajabu.

“Dunia yenyewe vitabu vya Mwenyezi Mungu vinasema aliumba mbingu na nchi kwa siku sita ya saba akapumzika, sasa kama Mungu anaumba kwa siku sita mpaka anataka likizo itakuwa sisi.

“Sisi tunafanya hatua tunapunguza matatizo au tunaondoa matatizo halafu tunaleta maendeleo na maendeleo yanazaa matatizo mapya hakuna unaweza kusema leo matatizo yote yamekwisha, wewe nawe utakuwa umekwisha lakini sio matatizo yataendelea kuwepo.”

Alifafanua ndio maana Chama Cha Mapinduzi ni chama cha kudumu cha kupambana na matatizo ya kimaendeleo na ingekuwa matatizo yote yanaisha mbona wameandika Ilani na yeye(Wasira) alikuwa mjumbe wa kamati Ilani.

“Najua sitaki ila kuieleza hapa kwa sababu watu wa kuieleza watakuja kutuambia tumefika hatua yetu mpaka hapa, tumefanya vizuri sana lakini bado tuna matatizo na tuna majibu ya matatizo hayo.

“Kwa hiyo huyo anayefikiri kwamba Rais angemaliza matatizo yote na yeye ni mbunge hakuyamaliza yote pale kwake maana yako matatizo ya Rais,matatizo ya wabunge na yako matatizo ya madiwani.”

Alisisitiza na hakuna mtu anayemaliza yote ila tunawashukuru wakifanya mambo mazuri kama tunavyomshukuru rais wetu.Ametumia nafasi hiyo kumshauri yule mbunge tena ni rafiki yake sana ila yeye naye ameingia choo kisichokuwa cha kwake ange ‘cheki’ vizuri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here