Wanaotumia rushwa kusaka uongozi CCM kushughulikiwa

0

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitawachukulia hatua ikiwemo kuwaengua au kufuta chaguzi iwapo itabainika kuna wagombea wametumia rushwa ili kupata nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa Kikao Maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichoketi katika ukumbi wa NEC (White House), Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu alisema wanafuatilia kwa makini mwenendo wa chaguzi hizo na hawatasita kuchukua hatua kwa watakaobainika kukiuka taratibu za chama hicho.

Alisema, katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni, wamechukua hatua kwenye baadhi ya Jumuiya baada ya kuwepo kwa malalamiko ya matumizi ya rushwa, ambapo tayari chaguzi zaidi ya tano kwenye Jumuiya ya Vijana zimefutwa na nyingine tatu kwenye Jumuiya ya Wanawake zimesimamishwa na bado wanaendelea kupokea malalamiko mengine.

“Halmashauri Kuu CCM imeagiza kusimamia haki na kukemea vikali matumizi ya rushwa kwenye chaguzi hizi zinazoendelea, na hatutasita, zipo chaguzi kwenye Jumuiya zimefutwa, kila penye malalamiko tutasikiliza, na pale ambapo itabainika kanuni na taratibu zimekiukwa, taratibu za kufuta au kutengua matokeo hayo zitafuatwa,” alisema Shaka.

Shaka alisema, kwenye chaguzi hizo ndio msingi unajengwa, hivyo ni vema Katiba na kanuni zikaheshimiwa ili kuwapata wagombea sahihi ambao watakuja kukisaidia chama kwenye chaguzi zijazo ukiwemo uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vitongoji unaotarajia kufanyika 2024 na uchaguzi Mkuu wa 2025 wa Rais, wabunge na madiwani.

“Chaguzi hizi ndio tunajenga msingi ambao utakwenda kutuvusha kwenye chaguzi zijazo, kwahiyo chama kinafuatilia kwa karibu sana mwenendo wa chaguzi hizo, kila ambako haki imepindwa, tutahakikisha haki inasimamiwa,” alisisitiza Shaka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here