Na Iddy Mkwama
HIVISASA mitaani, kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, gumzo ni kuhusu simulizi za mateso wanayoyapata wananchi baada ya kuchukua mikopo ambayo inajulikana kwa jina la ‘kausha damu.’
Mikopo hiyo imesababisha familia nyingi kusambaratika baada ya ndoa kuvunjika. Ipo mifano mingi ya akinamama ambao wamejiingiza kwenye mikopo kwa siri bila kuwashirikisha wenzi wao, wakiamini wanaweza kulipa.
Lakini, kinachotokea ni kwamba, wanashindwa kulipa mikopo hiyo na hatimaye siri inafichuka na kusababisha kukosekana kwa maelewano na hivyo kufikia hatua ya kuachana au kutengana.
Mbali na kusambaratika kwa familia, mikopo hii imekuwa chanzo cha watu kuwa maskini baada ya kupoteza mali zao zinazochukuliwa na taasisi za fedha iwapo mkopaji ameshindwa kurejesha mkopo.
Si hivyo tu, wapo watu waliopoteza maisha kwa mshtuko baada ya kufilisiwa mali zao, pia lipo tukio moja la mwanaume ambaye aliuawa kwa kipigo kutoka kwa watendaji wa kampuni moja ya mikopo ambayo ni maarufu kwenye mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Inadaiwa, mwanaume huyo hakuwa na taarifa za mkewe kukopa na katika harakati za kuzozana na watu hao ambao walitaka kuchukua vitu kwa ajili ya kufidia deni lao, wakashambulia na kusababisha kifo chake.

Kuanzia hapo, ndipo Serikali ikaamua kutupa jicho kwenye uendeshaji wa shughuli hizo za ukopeshaji ambazo zimeshamiri hapa nchini na tukasikia wamechukua hatua ya kuzifungia kampuni ambazo zilikuwa zinatoa mikopo bila kusajiliwa.
Ukweli ni kwamba, kampuni nyingi au wakopeshaji binafsi waliotapakaa mitaani, lengo lao kubwa sio kuwakwamua wananchi wa hali ya chini wakiwemo wajasiliamali, bali ni kutaka kuwapora mali zao wanazoweka dhamana ili wao waendelee kutajirika zaidi.
Ndio maana, sio jambo la kushangaza kusikia mtu amekopa Shilingi 500,000, lakini analipa mara tatu ya kiwango hicho na kadri anavyochelewa kulipa, kiwango kinaongezeka na hatimaye anashindwa kulipa hivyo anaamua kukimbia na kutelekeza familia au kufilisiwa.
Yote haya yanatokea kutoka na ukweli kwamba, wananchi walio wengi wanakwepa masharti magumu yanayotolewa na mabenki, ndio maana wanaamua kuchukua mikopo inayotolewa mitaani.
Vile vile, hawana taarifa kuhusu uwepo wa taasisi za Serikali ambazo zinatoa mikopo kwa masharti nafuu na riba ndogo, huku zikiangalia zaidi kuwainua kiuchumi wananchi wa chini.
Moja ya taasisi hizo ni Mfuko wa SELF (SELF MF), ambayo ni taasisi ya Serikali ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha, inayojishughulisha na utoaji wa mikopo kwa wananchi hasa wa kipato cha chini, wanaojishughulisha na uzalishaji mali ili waweze kujiongezea kipato na kupunguza umaskini.
Mfuko huu ulianza kutekeleza majukumu yake Julai 1, 2015, ukichukua majukumu ya mradi wa Serikali uliojulikana kama Small Loan Facility (SELF), mradi huu ulitekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka 15 kuanzia mwaka 2000 hadi 2015.
“Sisi ni taasisi ya huduma ndogo za fedha inayoongoza katika kubadilisha maisha ya watu. Tunawapa wananchi fursa ya kufanya kazi kwa kutoa huduma ndogo za fedha kwa masharti nafuu,” anasema Santiel Yona, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF.

Mtendaji Mkuu huyo, alizungumza hayo wakati wa mkutano na Wanahariri na Waandishi wa Vyombo vya habari, uliofanyika Agosti 15, 2025 jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina.
Anasema, katika utoaji wa huduma wanazingatia uadilifu, ushirikiano, ubunifu, kuzingatia mteja na uwajibikaji, mambo ambayo yanaufanya mfuko huo uwe kimbilio kwa wananchi wa hali ya chini.
Akitaja majukumu ya mfuko huo, Santiel anasema ni pamoja na kutoa mikopo midogo kwa watu binafsi, vikundi na taasisi ndogo za fedha zinazolengwa na Serikali ili kulea na kukuza sekta ya huduma za fedha kwa ajili ya kupunguza umaskini.
Jukumu jingine ni kutambua, kuendeleza na kukuza fursa za kuwezesha ajira kwa wajasiliamali wadogo na taasisi za huduma ndogo za fedha.
“Pia, jukumu letu jingine ni kuandaa na kuweka utaratibu na mikakati ya kuwasaidia wajasilimali wadogo ili kuwawezesha kupata huduma za kifedha kwa ajili ya kujiajiri,” anasema Santiel.
Mbali na majukumu hayo likiwemo kubwa la utoaji wa mikopo, Mtendaji Mkuu huyo anasema, wanatoa elimu ya fedha na kuwajengea uwezo taasisi za huduma ndogo za fedha na wateja mmoja mmoja nao wanafikiwa kwa ajili ya kujengewa uwezo wa kuendesha taasisi zao.

Aidha, anasema Mfuko wa SELF ambao una matawi 12 nchini, unatoa huduma za uwakala wa bima “tunahamasisha wananchi kujikinga na majanga kwa kukata bima, kuna bima ya mkopo na bima za kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali,”
Kwa upande wa aina za mikopo wanazozitoa, Mtendaji Mkuu wa SELF MF anasema, ipo mikopo kwa taasisi za huduma ndogo za fedha (MFI/SACOS) ambapo mikopo hii inalenga kuwanufaisha wanaofanya biashara au kilimo.
Pia, ipo mikopo ya moja kwa moja kwa wanufaika ambayo hii walengwa ni wajasiliamali wadogo na wa kati (MSMes), wakiwemo wakulima wadogo, wafugaji “tunawawezesha kuboresha makazi, nishati safi ya kupikia na mikopo kwa ajili ya watumishi wa umma.”
Kupitia mkutano huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa SELF, alitaja mafanikio ambayo yamepatikana kuanzia Juni, 2021 hadi 2025. Mosi;- Kuongeza upatikanaji wa huduma za mikopo kwa wananchi wa kipato cha chini (Financial inclusion).
“Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 mpaka kufikia Juni 30, 2025 mfuko umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 196.9 na kiwango cha mikopo chechefu kikiwa chini ya 10% na pia mfuko unajiendesha kwa faida,” anasema.

Anaendelea kusema, mikopo hiyo imewanufaisha watu 183, 381 ambapo kati yao wanawake ni 97,170 sawa na asilimia 53 na wanaume 86,211 sawa na asilimia 47.
Pili, anasema wamefanikiwa kukopesha na kujenga uwezo wa taasisi za huduma ndogo za fedha (MFIs), ambapo toka 2021 hadi 2025, wamezijengea uwezo taasisi 549 za huduma ndogo za fedha na hivyo kupunguza changamoto za uendeshaji wake.
Tatu, Mfuko wa SELF umesaidia kutengeneza ajira kwa wakopaji wao wenyewe na wale wanaowaajiri, ambapo ajira 183,381 zimetengenezwa kutoka mwaka 2021 hadi Juni 2025.
Nne, Mfuko wa SELF umeanza kutoa mikopo kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, ambayo ni ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Kama tunavyojua Serikali ina ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, nasisi tumeanza kutoa mikopo kwa ajili ya mkakati huo ambapo tumetoa mikopo kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia,” anasema.

Tano, kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi Juni 2025, mfuko huo ulifanikiwa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wapatai 10,378, ikiwa ni katika harakati za kutelekeza moja ya huduma wanazozitoa.
Pamoja na mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa SELF Santiel Yona anasema, wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo wananchi wengi kutokuwa na elimu ya fedha.
“Hii inachangia kukosa uelewa wa kutosha wakati wa kufanya maamuzi ya kukopa mikopo au kutumia mikoponje ya malengo yaliyokusudiwa,” anasema na kuongeza, changamoto nyingine ni wananchi wengi kutokuwa na utamaduni wa kukopa na kurejesha mikopo kwa hiari.
“Kuna changamoto nyingine ya wananchi wa kipato cha chini kuishughulisha na biashara zisizo rasmi, hii inaleta ugumu katika kuwakopesha,” anasema Santiel.
Hata hivyo, anasema licha ya changamoto hizo, wamejiwekea malengo matatu ili kutimiza majukumu yao kwa ufanisi. Mosi;- Kuwafikia wateja wengi zaidi hasa wa kipato cha chini na kutoa elimu ya fedha.
Anasema, katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2026-2030), mfuko unapanga kutoa mikopo ya Shilingi Bilioni 300 na kuwafikia wanufaika 200,000 na kuongeza matawi kutoka 12 hadi 22 kufikia 2030.
Pili, wamepanga kuongeza ufanisi ili kutoa huduma bora na kwa wakati, ambapo watahakikisha wanabadilisha mifumo na kutumia teknolojia.
Tatu, watahakikisha taasisi hiyo inakuwa endelevu kwa kusimamia utoaji wa huduma bora kuhakikisha mikopo inarejeshwa kwa wakati.
Hayo ndio malengo ambayo Mfuko wa SELF umejiwekea, ambayo naamini yatafikiwa kutokana na kasi ya ukuaji wake inayoonekana tangu ulipoanzishwa.
Naamini, iwapo mfuko huu kama unavyoendelea kujitanua na kujitangaza kwa wananchi na kuwafikia wengi zaidi, utakuwa mkombozi kwa watanzania wengi hususani wenye kiu ya kujikwamua na kutoka kwenye umaskini.
Mfuko huu ndio suluhisho pekee kwa wananchi wa hali ya chini ambao wanapata mateso makubwa kwa kulipa mikopo yenye riba kubwa, inayowadhalilisha na kuwafanya wawe maskini zaidi.