WAKAZI wa Kijiji cha Kamasi, Kata ya Ilangala, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, wameanza kunufaika na huduma za mawasiliano kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa na Kampuni ya Vodacom kwa ruzuku iliyotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Wananchi takribani laki nne (400,000) wanaoishi katika kata hiyo sasa wanapata huduma za mawasiliano kwa uhakika zaidi. Aidha, Kampuni ya Yas nayo imeweka mitambo yake katika mnara huo, hatua inayowezesha wananchi kupata huduma za mawasiliano kupitia mitandao miwili.

Mnara huo ni miongoni mwa minara 758 iliyojengwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano, hususan katika maeneo ya vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Kupatikana kwa huduma hizo kunachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi kwa kuwawezesha wananchi kufanya biashara kwa urahisi, kupata taarifa za masoko na huduma za kifedha kidijitali.
Vilevile, huduma za mawasiliano zinaboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kama elimu na afya, kurahisisha mawasiliano ya dharura, na kuimarisha usalama katika jamii.
