Wanaharakati wana ajenda nyingine zaidi ya kesi ya Tundu Lissu

0

Na Ahmad Mmow

KUNYAMAZA ni jibu kwa mpumbavu, vijana wa Kenya kuweni watundu badala ya utukutu.

Upo msemo wa wahenga unaosema, kunyamaza ni jibu pia kwa mjinga. Lakini pia ni jibu kwa mpumbavu.

Nafuatilia mitandaoni kinachoendelea baada ya wanaojiita wanaharakati waliorejeshwa katika nchi walizotoka. Ni baada ya kuzuiliwa uwanja wa ndege na wengine kushikiliwa kwa muda mchache na vyombo vya ulinzi na usalama vya hapa nchini.

Inasemekana kwamba, dhamira ya hao wanaojiita wanaharakati ni kutaka kushiriki na kuhudhuria kesi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Baada ya watu hao kurejeshwa makwao akiwamo mwanasheria na mwanasiasa wa Kenya, Martha Karua yamesemwa mengi.

Hata hivyo, baadhi ya watu hasa vijana wa nchi jirani ya Kenya ambao ni ndugu zetu, wamekwenda mbali na kuvuka mipaka ya utu na sitara ya ubinadamu.

Hakika mitandaoni, hasa mtandao wa tiktok kuna mambo machafu yasiyo mithilika, wanasema na wanafanya. Wanamtukana na kumkejeli Rais na Amiri jeshi mkuu wa Tanzania, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Vijana hao licha ya matusi yote na kejeli zote, lakini watanzania tumebaki kimya kiasi cha wenyewe kuuliza, kwanini hatujibu matusi na kejeli hizo?

Kwa hakika, wanachofanya sio matusi kwa Rais tu bali kwa watanzania wote. Kwani, Rais Samia hakukalia kiti hicho kupitia wala hakufanya mapinduzi. Bali amechaguliwa na wananchi kwa mujibu wa Katiba.

Baadhi yao kwenye ‘clip’ wanadai Rais wetu hakuchaguliwa. Ni ujinga na upumbavu wa kiwango kisicho na kifani kusema na kudhani hivyo.

Wale wote wenye fikra kama hizo ambao wengine wapo hata humu nchini, ni wajinga na wenye kupumbaa kiakili.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi Mkuu wa 2020 alikuwa mgombea mwenza wa hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Alipita na kuomba kura akiwa mgombea mwenza. Kitendo cha kumpigia kura hayati Dkt. Magufuli ni kumpigia kura Dkt. Samia.

Ndio sababu kwenye karatasi za kupigia kura kulikuwa na picha hayati Dkt. John Magufuli na Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwahiyo, alipofariki Dkt. Magufuli nafasi yake ilishikwa na Dkt. Samia ambae alichaguliwa na wananchi kupitia kura alizopigiwa hayati Magufuli; kura ambazo yeye alijiombea kupitia kwa mgombea wake wa urais.

Iwapo sisi wananchi tusingemtaka Dkt. Samia Suluhu Hassan tusingempigia kura na kumchagua Dkt. Magufuli, lakini kitendo cha kumpigia kura Dkt. Magufuli, ni sawa na kumpigia Dkt Samia. Ipo wazi kabisa hiyo. Wala haihitaji ‘D’ mbili kuelewa.

Kwahiyo, wanapotokea mabaradhuli kusema Dkt. Samia hakuchaguliwa na wananchi, ni zaidi ya uzumbukuku. Kuweni na adabu na wananchi tuliomchagua!

Sasa baada ya kujua ukweli huo. Ni dhahiri wanaomtukana na kumkejeli Rais Samia wanatutukana wananchi wote takribani Milioni 62 Kama kuna wanaounga mkono matusi na kejeli hizo, wajue wanaunga mkono kutukanwa.

Licha ya yote hayo, vijana wa Tanzania wapo kimya. Sio kwamba hawawezi kujibu matusi hayo. La hasha, bali ni kutokana na malezi bora na mema waliyopata kwa wazazi wao na waasisi wa taifa hili.

Bila shaka, wanakumbuka na kuzingatia msemo huo wa wahenga. Hongera sana vijana na wananchi wenzangu. Kwani mwenda wazimu akikukwapua nguo huwezi kukimbizana nae. Kwani nawe utaonekana ni mwendawazimu pia. Na katika hilo tumefanikiwa. Maana hata wenyewe wanahoji kwanini hatujibizani nao?

Mara kadhaa katika ‘clips’ zao wanadai wao ni wasomi kuliko watanzania. Pia, kwao nchini Kenya kuna Uhuru na demokrasia kuliko Tanzania.

Sisi watanzania tunambua vema kwamba, Uhuru bila mipaka hugeuka fujo. Ndicho ambacho ndugu zetu walichonacho sasa. Ni Uhuru gani wakumtukana na kumkejeli Rais wao kila uchao? Kwanini walimchagua awaongoze kama walikuwa hawamtaki? Kwahiyo Kenya hakuna demokrasia, bali kuna midomo-ghasia na fujo tu.

Nilitaraji kama ni wasomi wangekuwa watundu katika karne hii ya sayansi na teknolojia. Kujiita wasomi wakati hakuna hata jambo kubwa walilovumbua kutokana na elimu zao ambazo zingechagizwa na utundu ni ubwege.

Kinachoonekana ni kwamba vijana waKenya ni watukutu wasio na nidhamu wala adabu. Utamaduni ambao wanataka watanzania tuwe nao.

Ndugu zangu! kama vijana hao wa Kenya wanamkejeli na kumtusi Rais wao watashindwa nini kuwatusi ma Rais wa nchi jirani?

Ni jambo lisilowezekana kwa mtoto asie waheshimu na kuwatii wazazi wake tutarajie anaweza kuwa tii na kuwaheshimu wazazi wa watoto wa majirani. HAIWEZEKANI.

Kujinadi ni wasomi wakati wanaharibu uchumi wao wa nchi ni ujinga wa kupindukia. Hivi walipoharibu mali za serikali walimkomoa nani? Kwenda bungeni na kula makombo ndio usomi wenyewe? Rais Ruto angali ni Rais wao. Vipi mali walizoharibu? Ni upumbavu mkubwa.

Hata kama ingekuwa ni kweli, wanaharakati hao hawakutendewa utu. Lakini kwa usomi wao njia ni kutukana na kukejeli mamlaka ya nchi nyingine? Maana ya usomi na kuelimika vipo wapi hapo!!

Ebu tujiulize hao wanaharakati ilikuwa ni lazima washiriki na wahudhurie mahakamani wakati kuna uwezekano wa kufuatilia kesi hiyo kupitia mitandaoni?

Kwa madai yao ni kwamba, wanataka kusaidia ukombozi kwetu sisi wananchi wa Tanzania. Kana kwamba tunapigania Uhuru. Huku wakijua kwamba Tanzania ni nchi huru ambayo ina Katiba yake na sheria zake.

Kwa kumbukumbu zangu, Tanzania na Kenya haziwezi kulingana wala kufanana kwa huruma na upendo kwa nchi nyingine za Afrika.

Wakati wa kupigania Uhuru kutoka kwa wakoloni na mabeberu, sijaona katika historia kama Kenya ilijitolea kusaidia ukombozi wa nchi nyingine za Afrika.

Hali hiyo ni tofauti na Tanzania ambayo ilijitoa muhanga kuzisaidia nchi nyingine. Hasa nchi za Kusini mwa Afrika.

Ofisi nyingi za wapigania Uhuru ikiwamo SWAPO, FRELIMO, ANC, MPLA na nyingine nyingi zilikuwa Tanzania. Vipi leo waKenya wajifanye ni wasaidizi wa ukombozi katika nchi zilizo huru? Nadhani wana agenda nyingine.

Tanzania tunaamini Wa Africa ni wamoja na ni ndugu. Ushahidi wa hilo ni wimbo wetu wa taifa katika ubeti wa kwanza tu tunaiombea baraka Afrika. Huwa tunamuomba Mungu aibariki Afriaa. Tena sio bara tu bali na watu wake.

Vipi waKenya wimbo wenu wataifa unatambua thamani ya bara la Afrika na watu wake? Kama jibu ni hapana, vipi leo mjifanye mna uchungu na nchi nyingine ili hali nchini mwenu mnabaguana kwasababu ya ukabila?

Ni jambo la kushangaza kusikia wanaharakati hao kusema walikuwa wanakuja au walikuja kusikiliza kesi ili kuona kama haki za binadamu zinazingatiwa.

Katiba yetu ipo wazi kabisa kwamba kila mtu ana haki mbele ya sheria. Ana haki ya kujitetea. Na chombo pekee cha kutafsiri sheria na kutoa haki ni mahakama.

Kuhusu kesi ya Tundu Lissu ipo mahakamani. Kwetu sisi mahakama ni mmoja wa mihili mitatu ya utawala. Sasa ni haki gani ambayo Lissu hajapewa kiasi cha wanaharakati kufuatilia? Bila shaka wana agenda nyingine.

Katika hali nyingine yakushangaza vipi akina Martha Karua hawakemei udhalilishaji utu na ubinadamu unaofanywa na vijana wa nchi yake ya Kenya kwa Rais Dkt. Samia? Kwani Rais wetu sio binadamu? Bila shaka Martha Karua ni mtukutu kama hao vijana.

Iwapo Martha Karua anashindwa kukemea matusi na kejeli kwa Rais wetu, bila shaka nae ni mtukutu. Kwani haki za binadamu ni kwa wote.

Wahenga waliwahi kusema, asie funzwa na mamae hufunzwa na ulimwengu. Watoto wa Kenya wamelelewa vibaya na viongozi wenu ambao ni kama wazazi. Sasa tusishangae wakifunzwa na ulimwengu. Huku sio kwa hao wanaowalea vibaya na kuwadekeza. Walichokipata watukutu wanaojiita wanaharakati ni funzo toka kwa walimwengu.

Nirudie kuwasihi wa Kenya waache utukutu, wawe watundu ili maarifa yao yapeleke taifa lao mbele kimaendeleo na uchumi.

Aidha, naendelea kuwasihi vijana wa Tanzania na watanzania wote wenye mapenzi mema na uzalendo kwa nchi yetu kuendelea kuwa watulivu na ukimya. Kwani hao wenzetu nia yao sio njema na wanataka kututoa nje ya reli.

Hatuna sababu ya kujibizana nao. Ila kama watadiriki kuingia humu nchini basi wembe ni ule ule. Lakini, kama ni kubweka tu, acha wabweke.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here