OR- TAMISEMI
JUMLA ya wanafunzi zaidi 7000 wanatarajiwa kushiriki katika Mashindano ya UMITASHUMTA mwaka huu, yatakayoanza Juni 7, 2025 mkoani Iringa.
Kwa mara ya kwanza mashindano ya ya UMITASHUMTA & UMISSETA mwaka huu yatahusisha mchezo wa Kriketi, utakaoshirikisha wanamichezo kutoka mikoa ya Dodoma, Tanga, Morogoro na Dar es Salaam.
Akizungumzia maandalizi ya mashindano hayo, Mratibu wa Michezo hiyo, Yusuf Singo, alisema maandalizi yamekamilika kwa kiwango kikubwa na wachezaji kutoka mikoa mbalimbali wanasubiriwa kuwasili mkoani Iringa kwa ajili ya kuanza mashindano hayo.
“Mashindano haya ni jukwaa muhimu la kuibua vipaji kwa vijana wetu. Tumejipanga vizuri kuhakikisha yanakwenda kwa mafanikio,” alisema Singo.
Michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na mpira wa miguu kwa wavulana na wasichana, netiboli, mpira wa wavu, goli, mpira wa miguu maalum kwa watu wenye ulemavu, riadha, tenisi, mpira wa kikapu, mpira wa mikono, sanaa za maonesho, pamoja na nidhamu na usafi.
Mashindano haya yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, Juni 9, 2025 katika viwanja vya Kichangani, mkoani Iringa.
Mashindano ya UMITASHUMTA (kwa shule za msingi) na UMISSETA (kwa shule za sekondari) ni sehemu muhimu ya kukuza michezo na malezi ya vipaji vya wanafunzi nchini Tanzania.