Walioteuliwa kusimamia uchaguzi watakiwa kuelewa Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo ya uchaguzi

0

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewaasa watendaji walioteuliwa kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Madiwani kwa Tanzania Bara kuhakikisha wanasoma na kuelewa kikamilifu Katiba, Sheria, Kanuni Taratibu na Miongozo ya Uchaguzi.

Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mbarouk Salim Mbarouk, ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa uchaguzi yaliyofanyika katika ukumbi wa Polisi Ziwani, Zanzibar.

Alisema, uchaguzi ni mchakato wa kikatiba unaojumuisha hatua na taratibu mahsusi za kisheria zinazopaswa kuzingatiwa kwa ufanisi, ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki wenye amani na kukubalika.

Ameeleza kuwa ufanisi wa uchaguzi hujengwa kupitia utekelezaji wa majukumu kwa uadilifu na weledi mkubwa, na kwa kuzingatia matakwa ya sheria.

Aidha, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kushirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria, na kuhakikisha wanajiepusha kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa wadau wa uchaguzi.

Amehimiza pia umuhimu wa kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum na kuweka mipango madhubuti itakayowezesha uchaguzi kufanyika kwa utulivu na usalama.

Amefafanua kuwa uteuzi wa watendaji hao umezingatia masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, na masharti ya Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inaipa Tume mamlaka ya kusimamia na kuratibu chaguzi hizo.

Jaji Mbarouk pia amesisitiza kuwa ajira za watendaji wa vituo vya uchaguzi zizingatie vigezo vya weledi, uzalendo, uadilifu na kuepuka upendeleo wa kindugu au kirafiki kwa watu wasio na sifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ofisi ya Zanzibar, Adam Juma Mkina, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watendaji hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kufuata katiba, sheria na taratibu zote za uchaguzi.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamewahusisha waratibu wa uchaguzi ngazi ya mikoa, vyuo vya mafunzo, wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao katika ngazi ya Majimbo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here