*Waziri Nape awapa `Tano’, kukutana nao rasmi
*Tume ya TEHAMA yaahidi kukuza bunifu za TEHAMA
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeahidi kuboresha mazingira ya kukuza bunifu za teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa kujenga vituo vinane vya kukuza bunifu za TEHAMA nchini ili kuhakikishia Watanzania hawaachwi nyuma na kasi ya ukuaji wa TEHAMA.
Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Mhandisi Sadath Kalolo aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Nkundwe Mwasaga wakati ya mapokezi ya vijana wa Tanzania walioibuka washindi wa tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya Huawei (Huawei ICT Competition), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Vijana hao, Dickson Mram, Matimu Mahimbo na James Magessa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliwabwaga washiriki wengine 470 kutoka zaidi ya nchini 49 zilizovuka hatua za awali za ushindani. Katika fainali walichuana kwa ubunifu na mafunzo ya vitendo kwa siku tatu kuanzia Mei 23 huko Shenzhen, China.
Alisema, ushindi huo wa kihistoria kwa vijana wa Kitanzania umelipatia taifa heshima kubwa na kutoa taswira kwamba, ushindi huu unaweka mwelekeo mzuri wa nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha kuimarisha mabadiliko ya kidijiti na kujenga uchumi wa kidijiti.
“Ushindi wenu si ni heshima kwenu bali ni heshima kwa taifa letu. Ninyi ni mashujaa wetu. Mmeandika historia kwenye tasnia ya TEHAMA kwa sababu mashindano haya ya TEHAMA ya Huawei ni moja ya mashindano makubwa na yenye ushindani mkubwa.
“Tunawapongeza sana vijana wetu. Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, ninapenda kuwapa salamu kutoka kwa Waziri wetu wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye kwamba amefurahishwa sana na ushindi huu na ameahidi kuonana nanyi mara atakaporejea nchini,” alisema Mhandisi Kalolo.
Aliongeza kuwa, vituo vitakavyotumika kukuza bunifu za TEHAMA vitajengwa kwenye Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Lindi na Mjini Magharibi, kwa upande wa Zanzibar.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa karibu zaidi na vyuo vikuu nchini, na wadau wengine kwenye sekta ya TEHAMA wa ndani na nje ya nchi, lengo likiwa ni kuhakikisha kasi ya ujenzi wa Uchumi wa kidigitali inapata msukumo wa karibu na pia kuifanya iwe shirikishi.