Wakulima Mbarali waipongeza Serikali kwa ruzuku ya mbolea

0

WAKULIMA wilayani Mbarali mkoani Mbeya wamepongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kutekeleza mpango wa utoaji mbolea za ruzuku.

Wamesema hatua hiyo imepunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija katika kilimo cha mpunga, jambo lililochochea ari ya kufanya kilimo kwa ufanisi.

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 5, 2025, na wakulima wa Skimu za Umwagiliaji Igomelo na Mwendamtitu katika mkutano uliofanyika na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen Nindi, ambaye yuko katika ziara ya kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Wakulima hao wamesema mpango wa ruzuku ya mbolea umeleta mapinduzi makubwa katika kilimo kwa kuwa umewapunguzia gharama za uzalishaji kwa misimu mitatu mfululizo na kuongeza mavuno. Wameeleza kuwa kabla ya mpango huo, walikuwa wakitumia fedha nyingi kununua mbolea hali iliyokuwa ikipunguza faida katika kilimo chao.

Wamebainisha kuwa, kwa sasa anaweza kuvuna kati ya magunia 30 hadi 45 kwa ekari moja, tofauti na kipindi cha nyuma ambapo mavuno yalikuwa duni kutokana na gharama kubwa za pembejeo. Ameishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuboresha upatikanaji wa mbolea kupitia mpango wa ruzuku.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbarali, Raymond Mweli, amewahakikishia wakulima kuwa mbolea za ruzuku zinapatikana kwa wingi na zinauzwa kwa bei elekezi.

Amewataka wakulima wote kuendelea kujisajili na kuhuisha taarifa zao kwenye mfumo wa kidigitali wa pembejeo za ruzuku ili kuendelea kunufaika na mpango huo.

Akizungumza na wakulima hao, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Stephen Nindi, amezitaka kampuni za mbolea nchini kuwa na programu endelevu za utoaji elimu kwa vitendo kupitia mashamba darasa ili kuwajengea wakulima uelewa wa matumizi sahihi ya mbolea.

Aidha, amezihimiza kampuni hizo kuendelea kusaidia kaya zenye nia ya kulima lakini hazina uwezo wa kugharamia pembejeo, ili kujenga jamii inayojitegemea kwa kilimo chenye tija.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here