MAKAMU wa Rais, Dkt. Philip Mpango, ameongoza uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, Mkoa wa Pwani, akisisitiza umuhimu wa kuwafichua wahujumu wa rasilimali za umma bila woga.
Pia, aliagiza viongozi wa mikoa kushirikiana na wakimbiza Mwenge kufanikisha utekelezaji wa miradi inayotarajiwa kukaguliwa, kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi.
Dkt. Mpango alisisitiza kauli mbiu ya Mwenge wa mwaka huu inayohimiza Watanzania kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025 kwa amani na utulivu, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kulinda misingi ya demokrasia.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Mwenge wa Uhuru unahamasisha mshikamano na maendeleo, huku Waziri wa Nchi, Ridhiwani Kikwete, akieleza kuwa mbio hizo zitapita katika mikoa 31 na halmashauri 195, zikimulika maovu kama rushwa na uzembe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alieleza kuwa mkoa huo umeendelea kupiga hatua kimaendeleo kwa kuwa na viwanda 1,535, vikiwemo vikubwa 128.
Aliongeza kuwa Mwenge wa Uhuru utafanya ziara ya zaidi ya kilomita 1,300 mkoani humo, ukikagua miradi 64 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.28.