KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Waziri amewataka wahandisi nchini kuchangamkia fursa ya kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kulifikisha taifa katika uchumi wa kipato cha kati cha juu.
Amesema hayo akiwasilisha mada kuhusu nafasi ya uhandisi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika Maadhimisho ya 22 ya siku ya Wahandisi Tanzania ambayo yenye kaulimbiu isemayo “Wajibu wa Wahandisi kuelekea Dira ya Maendeleo 2050” jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa sekta ya maji ni nguzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi na inahitaji ubunifu wa kihandisi ili kufanikisha miradi mikubwa kama ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji, mabwawa makubwa, na miundombinu ya umwagiliaji yenye ufanisi wa matumizi ya maji.
Amebainisha baadhi ya changamoto zinazohitaji mchango wa wahandisi katika sekta ya maji ikiwemo gharama kubwa za umeme kwenye miradi ya maji, uwezo mdogo wa ndani kujenga miradi mikubwa, na hitaji la viwanda vya ndani vinavyotengeneza dira za maji.
“Kuna fursa mpya za miradi tasnia ya Uhandisi inaweza kutekeleza:- Decentralized Smart Water System, Solar-Powered Desalination for Coastal and Island Communities, Wastewater-to-Resource Solution and Flood Resilience Engineering.” Mhandisi Mwajuma Amesema.
Amesisitiza kuwa Wizara ya Maji imeshaanza utekelezaji wa ujenzi wa gridi ya Taifa ya maji ambapo miradi mikubwa ya maji imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa katika maeneo yenye maji ya uhakika kama vile maziwa, mito, na mabwawa makubwa hivyo wahandisi wanaweza kushiriki katika kufanikisha maendeleo zaidi.
Ameongeza kuwa maji ni sekta wezeshi na ni kichocheo na nyenzo ya mageuzi na imepewa uzito katika kufanikisha dira ya Taifa ya 2050, kuwa na taifa lenye lenye uhakika na usalama wa maji kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.