VIJANA nchini wametakiwa kuwafichua wafanyabiashara wasio waadilifu ambao wanadiliki kuihujumu Serikali kwa kuwauzia wananchi Sukari kwa bei ya juu ambayo si bei elekezi.
Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Rehema Sombi alisema hayo wakati akifungua Mkutano mkuu wa UVCCM vyuo na vyuo vikuu Taifa unaofanyika mkoani Iringa katika chuo cha Ihemi kinachomilikiwa na Jumuiya hiyo.
Rehema alisema, vijana wanapaswa kuwa askari namba moja wa kuibua vitendo vinavyofanyika kwenye jamii ambavyo vinamuumiza mwananchi moja kwa moja.
Alisema, wapo baadhi ya wafanyabiashara wanaouza bidhaa ikiwemo sukari kwa kujipangia bei zao wenyewe huku wakiwaumiza wananchi na kupelekea wananchi kuichukia Serikali yao pamoja na chama kinachoiongoza Serikali.