WAFANYABIASHARA wadogo na wakulima katika Kijiji cha Msolokelo, Kata ya Pemba, Wilayani Mvomero, Mkoani Morogoro, wameanza kunufaika na huduma za mawasiliano baada ya kukamilika kwa mnara mpya uliojengwa na kampuni ya Vodacom kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Kupitia huduma za kisasa za 2G, 3G na 4G, wanapata urahisi wa kujisajili katika mifumo mbalimbali, kufanya malipo ya kielektroniki, kuwasiliana haraka na wateja, na kufungua masoko mapya kupitia simu zao.
Hii ni ishara halisi ya mafanikio ya Serikali, ambapo mawasiliano yamekuwa nyenzo ya kuendeleza ndoto za kibiashara, kuongeza kipato cha kaya, na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kijiji cha Msolokelo.