Vyombo vya habari vyatakiwa kuripoti uchaguzi kwa usahihi

0

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevihimiza vyombo vya habari nchini kuripoti kwa usahihi na kwa wakati kuhusu taarifa zote zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, wakati wa ufunguzi wa mkutano kati ya Tume na Wahariri wa Vyombo vya Habari.

Jaji Mwambegele alisema, vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya mpiga kura na taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya maamuzi ya msingi kwa uhuru na kwa amani.

Aidha, amewasihi Wahariri wa vyombo vya habari kutumia majukwaa yao kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu, utakayofanyika Oktoba 29, 2025.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Tume na vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na kwa kuzingatia sheria za uchaguzi.

Akitoa mada kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kufanikisha maandalizi na uendeshaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Ameongeza kuwa, katika nchi yoyote inayodhamiria kufanikisha jambo kubwa kama uchaguzi, vyombo vya habari ndio msingi wa kwanza, kwani kupitia kwao, wananchi hupata taarifa sahihi, zilizofanyiwa utafiti na kuhakikiwa.

Kailima alisema, bila ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari, juhudi zote za Tume katika kutoa elimu na taarifa kwa umma haziwezi kuwafikia walengwa.

“Maana yake kila kinachotolewa na Tume hakiwezi kuwafikia wananchi iwapo vyombo vya habari havitaamua jambo hilo lifanikiwe,” alisema.

Ameongeza kuwa wadau wote wa uchaguzi, vikiwemo vyama vya siasa, wanategemea vyombo vya habari kutoa taarifa zitakazowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here