Vyama vya siasa vyatakiwa kutathmini mienendo yao

0

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Sheria ambazo zinahitaji marekebisho madogo zitafanyiwa kazi haraka huku nyingine zitachukua muda kidogo kulingana na muda wa mchakato wa utekelezaji.

Rais Samia alisema hayo wakati akipokea Ripoti ya Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na Kikosi Kazi ni kuruhusiwa kufanyika kwa mikutano ya hadhara kwa mujibu wa Katiba na Sheria pamoja na kuzingatia 40% ya jinsi katika vyombo vya maamuzi vya vyama vya siasa.

Rais Samia ameunga mkono pendekezo la kufanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa kwani kutumia Sheria na Kanuni za awali zingeendelea kusababisha changamoto na dosari zilizokuwa zikijitokeza mwanzoni.  

Rais Samia pia amevitaka vyama vya siasa kutathmini mienendo ya vyama vyao hasa kuzingatia usawa wa kijinsia, matumizi mazuri ya fedha, utawala bora na kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake kugombea nafasi muhimu.  

Vile vile, Kikosi Kazi hicho kimependekeza utaratibu mpya wa kupata Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, utendaji wa Tume uruhusiwe kuhojiwa kwenye Mahakama ya Juu na pia isilazimike kufuata amri ya mtu yeyote, Idara yoyote ya Serikali, Chama chochote cha siasa au Taasisi yoyote.

Kikosi Kazi hicho chenye Wajumbe 24 na kilichowasilisha maeneo 9 ya kufanyiwa kazi, kimependekeza matokeo ya Uchaguzi wa Rais yahojiwe kwenye Mahakama ya Juu mara itakapoanzishwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here