Vigogo ACT Wazalendo wadaiwa kujiandaa kuhamia CUF

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

BAADHI ya vigogo ndani ya ACT Wazalendo wapo mbioni kurudi Chama cha Wananchi (CUF) kufuatia mwenendo usioridhisha wa viongozi wao ambao hivi sasa wanahaha Jijini Dar es Salaam, kutafuta ushirika na vyama vingine kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Duru za kisiasa ndani ya chama hicho zinabainisha kuwa, miongoni mwao wapo wabunge na wawakilishi wa chama hicho ambao inatajwa kuwa wanasubiri mafao yao ili wajiondoe ACT Wazalendo na kuelekea chama hicho ambacho awali kilikuwa na ushawishi mkubwa Visiwani Zanzibar.

Habari za ndani zinaeleza kuwa, vigogo hao hususan wale wa Zanzibar wameamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona ACT imepoteza ushawishi visiwani humo sababu kubwa ikitajwa kuwa ni mwenendo usioeleweka wa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Zanzibar Jussa Ismail Ladhu ambaye anashutumiwa kwa kuhubiri ubaguzi.

Mmoja wa wanachama wa chama hicho ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kuhofia ‘kushughulikiwa,’ alisema Jussa anaivuruga ACT Wazalendo kama alivyofanya kwa CUF kipindi kile na kubainisha licha ya wale ambao si viongozi, waliorejea chama hicho awali, pia kuna kundi jingine linalojumuisha wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar.

“Watu wanaona bora chama cha zamani (CUF), pengine kinaweza kuwa na hoja mpya, lakini hizi za Jussa na wenzake haziwezi kufanya wananchi wakafikiria kutupa kura,” alisema na kuongeza kuwa, uchaguzi wa mwaka huu 2025 huenda ukawa mgumu kwao kuliko chaguzi zingine.

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba akizungumza katika kipindi cha One on One kinachorushwa na Wasafi TV, mwishoni mwa wiki iliyopita, alikaririwa akisema kuna vijana wengi wanakuja katika chama hicho wakitokea ACT Wazalendo.

“Mfano Khatibu Ally ndio Katibu Mkuu wetu mpya kwa sasa, huyu alitimkia ACT Wazalendo lakini karudi, wengine waliwahi kuwa wabunge Bunge la Jamhuri ya Muungano Zanzibar kina Rajab Lanzi na viongozi wengine ambao hawajajitokeza,” alisema Prof. Lipumba.

Alisema, wapo wengi ambao wanaunga mkono juhudi za CUF na wengine ambao watajitokeza muda ukifika na hilo linaweza kuwa pigo kubwa kwa ACT Wazalendo ambacho wabunge wake wengi akiwemo Mbunge wa Konde, Pemba kwa tiketi ya chama hicho, Mohamed Said Issa (Konde).

Mbunge huyo wa Konde katika mahojiano na ITV katika kikao cha bunge kilichoahirishwa hivi karibuni, alikiri kutatuliwa kwa changamoto ya upatikanaji wa maji, hospitali ambapo wajawazito walilazimika kufuata huduma Micheweni wilayani au kujifungulia nyumbani, shule za ghorofa na uwekezaji wa ujenzi wa hoteli za kitalii.

Pia, mbunge huyo alikiri kuwa wapiga kura wake wanafurahi sasa kwani barabara ya kiwango cha lami imejengwa kutoka Konde hadi Micheweni ambayo awali ilikuwa mbovu na isiyopita kwa urahisi pamoja na huduma zingine za msingi.

Siku za karibuni Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Jussa Ismail Ladhu akiwa na Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu walikuwa Jiji ni Dar es Salaam kutafuta ushirikiano na vyama vingine kuelekea uchaguzi mkuu

Wachunguzi wa mambo wanadai kuwa, hatua hiyo ni dalili ya kwenda mrama kwa chama hicho hususan Zanzibar, na jambo baya zaidi baadhi ya vyama vimekataa ushirikiano huo, hoja ambayo wanaona imeibuka ghafla na hakuna maandalizi ya maana wala kujua kusudio lake la msingi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here