Uzalishaji wa takataka waongezeka

0

UDHIBITI wa takataka ni mojawapo ya changamoto kubwa za kimazingira zinazoikabili nchi na uzalishaji ukiongezeka kwa kiwango cha tani Milioni 14.4 – 20.7 kila mwaka, huku Mkoa wa Dar es Salaam ikizalisha 15.3% ya jumla ya taka.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameyasema hayo katika zoezi la usafishaji wa Fukwe ya Bale katika Jiji la Dar es Saalaam, Mei 3, 2025 akieleza taka nyingi zinazozalishwa Dar es Salaam zinaishia baharini, hivyo kuathiri mazingira ya bahari.

Alisema, Ukanda wa Pwani wa Dar es Salaam sio tu ni mali muhimu ya kiuchumi na kiikolojia, bali pia ni chanzo cha burudani na fahari ya kitamaduni. Fukwe zenye afya huchangia katika utalii, uvuvi, na ustawi wa jamii za pwani.

“Kwa bahati mbaya, wanazidi kutishiwa na uchafuzi wa mazingira haswa taka za plastiki, hii ina maana kwamba hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kutatua changamoto na napenda kusisitiza kwamba Serikali bado ina nia ya dhati ya kuongoza usimamizi wa mazingira nchini, hivyo imefanya jitihada kubwa katika kutatua changamoto za udhibiti wa taka.”

Waziri Masauni alisema, moja ya jitihada zinazofanywa ni Uundaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira (2021) ambayo ni mfumo wa sera ya kushughulikia changamoto za mazingira ikiwa ni pamoja na usimamizi wa taka. Sera hiyo pia inatoa hatua za kimkakati kwa ajili ya kukuza ufumbuzi wa mzunguko wa udhibiti wa taka nchini.

“Maendeleo ya Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Mazingira kwa Afua za Kimkakati (2022- 2032). Mpango unaangazia changamoto za mazingira katika mifumo ikolojia tofauti na afua za kimkakati za kuzitatua, usimamizi wa taka ikiwa ni moja ya changamoto zilizoainishwa. Pia iliweka msisitizo mkubwa katika mbinu ya uchumi wa mzunguko wa usimamizi wa taka.

Aliongeza kuwa, Kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji wa Usimamizi wa Taka, unaofafanua kwa kina fursa za uwekezaji zinazopatikana katika sekta ya usimamizi wa taka. Kwa kuongezea, utekelezaji wa kutumia tena, kupunguza, na kuchakata tena kumechochea uwekezaji katika sekta hiyo, kwani zaidi ya kampuni 257 za ndani na watu 99 hujihusisha na ukusanyaji, usafirishaji na urejelezaji taka ngumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here