‘Uwekezaji DP World umeleta ufanisi’

0

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema, uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam uliofanywa na kampuni ya DP World umeleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji na ufanisi mkubwa bandarini hapo kwa maendeleo na ustawi wa nchi.

Akizungumza mara baada ya ziara ya kutembelea bandari ya Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, Mohamed Kawaida ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kizalendo wa kuruhusu uwekezaji huo ambao una manufaa makubwa kwa taifa.

Alisema, ripoti ya utendaji iliyowasilishwa na uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) umeonesha kuongezeka kwa ufanisi na kazi ya upakuaji na usafirishaji wa mizigo bandarini hapo tofauti na hofu iliyokuwepo hapo awali na watu waliokuwa wanapinga uwekezaji huo.

“Tukiwa kama wasimamizi wa Serikali katika utekelezaji wa ilani ya CCM, tumeamua kutembelea bandari ya Dar es Salaam kujionea shughuli mbalimbali zinavyofanyika na kufurahishwa na ufanisi wake baada ya uwekezaji mkubwa kufanyika,” alisema Kawaida.

Alisema, lengo kubwa la ziara hiyo ambayo pia ilihusisha wenyeviti na makatibu wa UVCCM kutoka mikoa yote hapa nchini, lilikuwa kujionea na kujifunza namna kazi zinavyofanyika bandarini hapo.

“Mimi na viongozi wenzangu wote wa UVCCM tumefurahishwa na tija ya uwekezaji huu katika bandari ya Dar es Salaam,” alisema na kuongeza kuwa, awali kulikuwa na maneno mengi ya upotoshaji kwamba uwekezaji huo hauna tija kwa taifa na Watanzania wengi wangepoteza ajira na wafanyabiashara kukimbilia bandari nyingine za nchi jirani.

“Mwekezaji DP World amewekeza fedha nyingi katika miundombinu na vitendea kazi uliochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa shehena za mizigo katika bandarini,”

“Lakini katika ziara hii tumejionea hali tofauti kabisa, ambapo ufanisi na upakuaji mizigo umeongezeka baada ya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na vitendea kazi kufanyika,”

“Hii inamaanisha kuwa mapato yanayotokana na uwekezaji huu yameongezeka na kuwa na tija katika maendeleo ya nchi yetu,” alisema Kawaida na kuongeza kuwa, Tanzania imebarikiwa neema ya kuwa na bandari hiyo inayohudumia nchi mbalimbali zikiwemo Rwanda, Burundi, Congo DRC, Msumbiji na Zambia.

Alisema, uwekezaji kama huo ulihitajika ili kuendeleza kukuza soka la biashara katika bandari ya Dar es Salaam. “Dhana ya nchi yetu ni kuingiza kipato kwa maendeleo ya nchi kupitia maboresho ya sekta ya usafirishaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya reli ya SGR ambayo pia tumeitembelea na kuridhishwa na maendeleo yake.”

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa TPA, Plasduce Mbosa, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Selemani Mrisho alisema, viongozi wa umoja huo wamefurahishwa na ufanisi unaofanywa na mwekezaji DP World bandarini hapo kama ilivyotarajiwa na kujifunza mengi wakati wa ziara hiyo.

Alisema, ili kuleta ufanisi na tija, mwekezaji DP World ameweka vitendea kazi mbalimbali bandarini hapo katika kuhudumia shehena za mizigo bandarini na kufanya ufufuaji wa mashine (SSG)  ambazo hapo awali zilikaa muda mrefu bila kufanya kazi kwa sababu ya matatizo ya umeme.

“Sasa hivi mwekezaji anazalisha umeme kupitia mashine hizo. Pia, mwekezaji ameweka mashine za kuhudumia makasha katika uboreshaji wa miundombinu hiyo,” alisema.

Mrisho alitoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuitumia bandari hiyo kutokana na mageuzi makubwa yanayofanyika katika kuharakisha kazi ya upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini hapo. Ripoti ya utendaji kazi wa bandari hiyo iliyowasilishwa wakati wa ziara hiyo kwa viongozi wa umoja huo imeonyesha mafanikio makubwa  yamepatikana baada ya Serikali chini ya Rais Samia kuridhia uwekezaji wa DP World bandarini hapo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here