NI wazi kwamba, Watanzania bado wanatibu majeraha ya matukio ya vurugu yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana.
Athari za vurugu hizo bado zimegusa watu, mali na kuathiri uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa. Tulijikwaa kama Taifa na hatupaswi tena kufumbia macho viashiria vya kuvuruga amani, utulivu na umoja wa kitaifa.
Katika kipindi ambacho taifa linasubiri kupata matokeo ya uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, kumejitokeza wimbi la taarifa zisizo na uthibitisho, zikiwemo zilizoandikwa na kada wa Chadema na mwanaharakati Hilda Newton, kwa alichodai kueleza yaliyomo ndani ya ripoti ya awali ya Tume ya Jaji Mohamed Chande Othman.
Andiko la Newton linaibua maswali mazito, si kuhusu ukweli wa yaliyotokea Oktoba 29, bali kuhusu namna siasa zinavyoweza kutumika kupotosha ukweli na kujaribu kuathiri mchakato wa kitaifa unaoendelea.
Ukiyapitia kwa makini madai yaliyotolewa, unaona juhudi za makusudi za kueneza uzushi usio na ushahidi, kufanya propaganda ya kisiasa, na zaidi ya yote, jaribio la kuingilia uhuru wa Tume.
Msingi wa hoja katika andiko hilo ni madai yasiyothibitshwa kwamba Tume iliwasilisha ripoti ya awali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambayo imekataliwa kwa sababu za kisiasa.
Kada huyo anajaribu kuaminisha umma kuwa, kuna mvutano kati ya Tume na mamlaka za juu kuhusu maudhui ya ripoti hiyo. Haya ni madai mazito ambayo hata akiombwa kuthibitisha, hawezi kuyathibitisha. Hana ushahidi wa kuonesha uwepo wa maelekezo hayo, mawasiliano hayo, wala maudhui ya ripoti yenyewe.
Anachojaribu kufanya ni kueneza taarifa zisizo sahihi ili kuchochea mjadala wa umma unaoweza kuwafanya baadhi ya Watanzania kupoteza imani na mchakato unaoendelea. Hii si mbinu sahihi na yenye nia ovu katika wakati ambao Taifa linatafuta suluhu ya kudumu ya changamoto za kisiasa na uhalifu dhidi ya watu na mali uliojitokeza wakati wa uchaguzi.
Uzushi huu wenye mrengo wa kisiasa unakusudia kujenga hisia hasi na kupotosha ukweli kuhusu mchakato wa uchunguzi na matokeo yake kwa manufaa ya kisiasa. Hili halipaswi kufumbiwa macho, hasa kwa Watanzania wanaothamini amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Tabia ya baadhi ya wanasiasa na wafuasi wao kuendelea kuzua na kuchochea taharuki ni hatari kwa juhudi za kutatua changamoto zilizojitokeza na kujenga msingi mzuri wa maridhiano nchini, ambayo bila shaka ni kiu ya wananchi wengi nchini.
Ni ukweli ulio wazi kuwa Tanzania imekumbwa na changamoto kubwa kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025. Hakuna anayepaswa kupuuza yaliyotokea. Hata hivyo, hakuna taifa lisilo na changamoto—aidha za kisiasa, kiuchumi au kijamii.
Hata Mataifa yaliyoendelea hukabiliwa na changamoto lukuki, lakini ukomavu wao na wa watu wao unawasaidia kuvuka bila kuhatarisha mustakabali wa mataifa yao.
Uimara wa taifa hupimwa kwa namna linavyokabiliana na changamoto hizo. Ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan, kwa mujibu wa Katiba, aliunda Tume ya Jaji Othman Chande ili kuchunguza kwa kina matukio ya kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Tume hii inajumuisha wajumbe wenye taaluma na uzoefu mkubwa katika utumishi wa umma, kutoka mihimili mbalimbali ya dola, ikiwemo mahakama, serikali na diplomasia. Ni vigumu kutilia shaka uzalendo na weledi wao.
Madai kuwa Tume inaelekezwa au kushinikizwa ni jaribio la kudhoofisha imani ya umma, kuathiri mchakato wake, na kuandaa mazingira ya kukataa matokeo yake kabla hayajatolewa.
Ni wazi kuna baadhi ya watu, hususani wanasiasa na wafuasi wao, wanatamani kuona kazi ya Tume ikikwamishwa kwa masilahi yao binafsi. Hata hivyo, hakuna masilahi ya mtu au kundi yanayoweza kuzidi masilahi ya taifa.
Cha kusikitisha, ingawa si jambo la kushangaza, andiko hilo linatumia lugha ya kubeza, dhihaka na hisia kali. Hali hii si ya bahati mbaya. Katika mawasiliano ya kisiasa, hoja inapokosa msingi wa ushahidi, mara nyingi hubadilishwa kuwa kejeli, hasira na mashambulizi ya maneno kwa lengo la kudhalilisha wale wanaotofautiana kimtazamo, kiitikadi au kwa hoja.
Ni jambo linalotia wasiwasi kuona kiwango kikubwa cha kupungua kwa maadili, utu, heshima, busara na hekima miongoni mwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati. Endapo mwenendo huu utaachwa uendelee, unaweza kudhoofisha misingi ya maadili na utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika, na hivyo kuhatarisha mustakabali wa jamii.
Kwa upande mwingine, andiko la Hilda linajaribu kupandikiza hofu na taharuki kwa umma kwa kuibua madai ya uwepo wa majeshi ya nje yaliyodaiwa kuhusika na vifo vya raia wakati wa vurugu za Oktoba 29.
Madai haya, yanapotolewa kwa kurejea ripoti ya Tume ambayo bado haijakamilika, yanaashiria dhamira ya kuchochea hofu miongoni mwa wananchi, kudhoofisha imani kwa taasisi za dola na kuvuruga utulivu wa kijamii ambao umeanza kurejea baada ya matukio hayo yaliyoathiri baadhi ya mikoa nchini.
Taarifa za baadhi za askari kuua raia, takwimu za vifo na wahusika wa ghasia za uchaguzi zinalenga kushinikiza mitazamo kabla ya ukweli kujulikana, Kujaribu kuweka hitimisho kabla Tume haijakamilisha kazi yake ni kinyume na misingi ya haki.
Jukumu kubwa la Tume limekuwa kukusanya Ushahidi, kusikiliza pande zote na kutoa hitimisho huru. Kuisukuma Tume ichukue msimamo fulani kupitia shinikizo la kisiasa ni kuingilia uhuru wake.
Kujaribu kuaminisha umma kuhusu kilichomo ndani ya ripoti ya Tume kabla hata kazi haijakamilika ni muendelezo wa propaganda za kisiasa zenye nia ovu ya kuendelea kuitikisa nchi, mamlaka za utawala na taasisi zinazohusika na haki, ulinzi na usalama nchini.
Kujaribu kuweka hitimisho kabla Tume haijakamilisha kazi yake ni kinyume na misingi ya haki. Jukumu la Tume ni kukusanya ushahidi, kusikiliza pande zote na kutoa hitimisho huru.
Katika mazingira haya, ni muhimu kutoa rai kwa wanasiasa, wanaharakati na Watanzania wanaoitakia mema nchi yao kuacha kusukumwa na misingi ya kiitikadi na masilahi binafsi, na kuepuka kusambaza taarifa zisizo na ukweli au zisizo na uthibitisho.
Ni muhimu kutambua kuwa siasa za ushindani zinapaswa kuimarisha uwajibikaji kwa kila upande, na hazipaswi kuwa sababu ya kupotosha ukweli au kuchochea taharuki, chuki na uhasama katika taifa.
Ni vema Tume ya Uchunguzi iachwe ikamilishe kazi yake kwa uhuru. Ina watu wenye weledi, uzoefu na uzalendo wa dhati kwa taifa hili, na tayari makundi mbalimbali yameshiriki kutoa taarifa na ushahidi kuhusu matukio ya Oktoba 29. Matokeo yake yatakuwa na msingi wa haki ikiwa mchakato wake utaheshimiwa na kila mmoja wetu katika kutafuta ukweli wa changamoto zinazoikabili nchi.
Amani na utulivu wa Tanzania ni mtaji mkubwa wa taifa. Havipaswi kuchezewa kwa maneno ya kisiasa, propaganda au simulizi zisizo na ushahidi, wala zile zenye lengo la kuzua hofu, taharuki, chuki, visasi na uhasama miongoni mwa Watanzania.
Katika kipindi hiki muhimu, taifa linahitaji utulivu zaidi kuliko kelele, ukweli kuliko propaganda, na subira kuliko siasa zenye misukumo hasi. Mjadala unapaswa kujikita katika ukweli na mchakato uliotumika kuupata ukweli huo, ambao, kama ilivyo desturi ya haki, utapatikana kupitia mchakato huru, si kwa mashinikizo au propaganda za kisiasa.