Ukwasi tunao na mtaji tunao – TCB

0
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo.

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imesema ina ukwasi na mtaji wa kutosha kuwawezesha wateja wao kwa makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara ambao ni moja ya maeneo ya kimkakati yanayopewa kipaumbele.

Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB Adam Mihayo alisema hayo jijini Dar es Salaam na kuweka wazi kwamba, miongoni mwa vitu vilivyochochea ongezeko la ukwasi huo ni ubunifu walioufanya wa kuanzisha huduma ya kusimamia fedha za vikundi vya kijami kupitia M-Koba kwa kushirikiana na Kampuni ya simu.

Alisema, ushirikiano huo umewawezesha kukusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 80, hivyo wanapata uwezo zaidi wa kuwawezesha wafanyabiashara katika kukuza mitaji yao. “pia Benki Kuu imekuwa ikitupa ukwasi.”

Mihayo akizungumzia uimara zaidi wa benki hiyo alisema, katika kipindi cha robo ya mwaka 2024 imetengeneza faida ya Shilingi Bilioni 10.7 baada ya kodi. Faida hiyo ni ongezeko la asilimia 529 ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 1.7 kwa kipindi kama hicho mwaka 2023, huku ikitarajia kukusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 40.

Alisema, faida kabla ya kodi ilikuwa Shilingi Bilioni 13.6 kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu ambayo ni sawa na asilimia 353, huku amana za wateja wa benki hiyo zimeongezeka kwa asilimia 12 kufikia Shilingi Trilioni 1.1 za kitanzania.

“Amana hiki ni kiashiria cha jinsi wateja wanavyokuamini, tumekuwa tukikua mwaka hadi mwaka, ni kitu kizuri na tunawashukuru sana wateja wetu kwa kuendelea kutuamini,” alisema.

Aidha, alisema mikopo kwa wateja imepanda kwa asilimia 15.4 kufikia Shilingi Bilioni 983.6 na katika robo ya kwanza ya mwaka ambayo imefikia tamati Machi 31, mwaka huu wana ongezeko la faida ya Shilingi Bilioni 10.7 baada ya makato ya kodi.

Alisema, mapato yameongezeka kwa asilimia 30 mpaka kufikia Shilingi Bilioni 56.8 za kitanzania yakiimarishwa na kitabu cha mizania na kasi kubwa ya ukuaji katika mapato yote. Pia, kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024 mapato yamefikia Shilingi Bilioni 56.8 kutoka Shilingi Bilioni 43.7 kwa kipindi kama hiki mwaka 2023.

“Tunataka tuwe namba tatu kwa upande wa mali, mikopo na ukwasi, tunataka upande wa gawio tuwe namba tatu, tunaamini kwa uwekezaji tuliofanya kwenye huduma za Kidijitali tutaongeza wateja na tutafikia lengo,” alisema Mihayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here