Ukitaka kuandamana kwa Amani Afrika utapata kibali?

0
Protesters run away from the police during clashes in Nairobi, Kenya May 16, 2016. REUTERS/Goran Tomasevic

Na Magoiga SN

MAANDAMANO yapo ya aina nyingi, mimi nimeyagawanya katika makundi matatu; maandamano ya amani, maandamano yasiyo ya amani na maandamano ya kimapinduzi.

Tukianza na maandamano ya amani, haya ni yale maandamano yenye kibali ambayo yanafanyika kwa kufuata taratibu zote za kikatiba, kisheria na kikanuni. Maandamano haya malengo na maudhui yake yanakubalika kikatiba na kisheria, lakini tatizo linakuja pale ambapo waandamanaji watanyimwa kibali.

Aina nyingine ni maandamano yasiyo ya amani, maandamano haya huzuka kutokana na sababu mbalimbali bila kufuata taratibu wala sheria, mara nyingi maandamano ya aina hii huweza kusababisha vurugu, uharibifu mkubwa na hata majeruhi au vifo.

Kwa ufupi maandamano yasiyo ya amani hayahitaji kibali maana waandamanaji huwa wamejitolea kuvunja sheria, na katika mazingira kama hayo, usishangae jeshi kuingilia kati na kutumia nguvu.

Vurugu nyingi husababishwa na ukweli kwamba, siyo kila aliye katika msafara wa waandamanaji lengo lake ni maandamano, wengine ni wahalifu wa kawaida wanaotafuta mwamvuli wa kufanya uhalifu wao kama kupora maduka, kupiga watu n.k. Vyombo vya dola duniani kote huingilia kati maandamano ya aina hii ili kuzuia yasifanyike, maana madhara yake huwa ni makubwa yasipodhibitiwa.

Maandamano ya kundi la tatu ni maandamano ya kimapinduzi, haya hufanywa na wananchi au kundi la watu linalotaka kupindua Serikali iliyopo madarakani kwa sababu wanazozijua wenyewe, wakifanikiwa huwa ni ushindi kwao, lakini wakishindwa mara nyingi huwa ni kilio kwao maana hutafsiriwa kama ni uhaini.

Lakini, mbali na maandamano ya kimapinduzi kuwa na lengo la kupindua Serikali, pia yanaweza kulenga kulinda Serikali iliyopo madarakani dhidi ya watu fulani, kama ilivyotokea Uturuki mwaka 2016 Julai.

Nchini Marekani wananchi wanaweza kufanya maandamano au mikusanyiko ya amani yenye lengo la kuipinga Serikali au kupaza sauti kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa, kimataifa, kijamii, kisiasa au kielimu. Siyo kupinga pekee, lakini pia wananchi wanaweza kufanya mikusanyiko au maandamano ya amani kuunga mkono masuala mbalimbali.

Pamoja na haki hiyo ya kikatiba ya kuandamana, bado kuna sheria na kanuni mbalimbali ambazo lazima zifuatwe kabla ya kuandamana iwapo maandamano yanaitwa ya amani.

Maandamano ya amani ni yale ambayo yamekidhi vigezo vyote vya kikatiba, kisheria na kikanuni. Pia ikumbukwe kuwa, lengo la maandamano ya amani siyo kuvunja sheria bali ni kuhakikisha waandamanaji wanafikia lengo lao kwa amani huku wakiwa wamefuata sheria.

Kila jimbo (State) la Marekani lina sheria na kanuni zake zinazosimamia suala la maandamano ya amani. Haijaishia hapo, wakati mwingine manispaa zinazojitegemea au majiji yanaweza kuwa na sheria zake zinazojitegemea kuhusiana na suala la maandamano (Protests and Demonstrations).

Hata hivyo, yapo mambo ambayo ni lazima yazingatiwe katika maandamano ya amani nchini Marekani, miongoni mwa mengi ni pamoja na kibali cha kuandamana, kwamba kabla ya kuandamana ni lazima mhakikishe kuwa mmepata kibali kutoka mamlaka zinazohusika.

Wakati Mange Kimambi alipohamasisha maandamano ya 26 Aprili, utakumbuka kuwa waliotaka kuandamana katika nchi kama Ujerumani, Uingereza, Marekani n.k walichokifanya kwanza ni kutoa taarifa ya lengo lao la kuandamana na kupewa kibali cha kuandamana kwa amani.

Unapoomba kibali cha kuandamana lazima utaje muda, tarehe na hata eneo ambalo unataka kufanyia maandamano yako, maana utoaji wa vibali huzingatia pia vigezo hivyo. Ukiomba kuandama siku ambayo mamlaka itaona kuwa itaingiliana na maslahi mapana ya wengine unaweza kunyimwa kibali, vile vile ukiomba kuandamana siku au eneo ambalo jeshi la polisi litaona haliwezi kutoa ulinzi wa kutosha unaweza kunyimwa kibali.

Kuna majimbo ambayo unahitaji kutoa taarifa na kupata kibali masaa 48 kabla ya muda unaotaka kuandamana. Jimbo la California unahitaji kutoa taarifa angalau siku 40 kabla ya siku unayotaka kuandamana.

Pia kwa kutegemea na eneo unalotaka kufanyia maandamano yako kama vile viwanja vya wazi au bustani na kila eneo lina utaratibu wake wa muda wa chini unaotakiwa kuomba kibali cha kutumia eneo husika kuandamana. Mfano huko Colorado ikiwa unataka kuandamana eneo la Denver Parks and Recreation unahitaji kuomba kibali siku 60 kabla ya siku yako unayotaka kuandamana.

Katika majimbo mengi nchini Marekani mfano Alaska, Albama, Arizona na Alkansas, kibali cha kuandamana kinalipiwa fedha (Non-refundable fee). Yaani unapojaza fomu ya kuomba kibali cha kuandamana, uandae na ada ya kulipia kibali husika. Kuna majimbo ambayo kibali cha kuandamana utakipata kwa kulipia $50 mpaka 300 kutegemea na jimbo.

Maandamano yako ya amani hayapaswi kuingilia shughuli za watu wengine ambao hawahusiki na maandamano hayo, yaani kwa mfano, iwapo unaandamana kwa amani huruhusiwi kuziba barabara za watembea kwa miguu, au hata kusababisha foleni kwa kuziba barabara za kupita magari.

Kiufupi maandamano yako hayaruhusiwi kuingilia shughuli za wengine, ndiyo maana huwa unaona watu wakiandamana Marekani wengine wanapita na kuendelea na shughuli zao.

Katika baadhi ya majimbo kama Alaska, ukijua kuwa maandamano ya amani unayoyaandaa yatahusisha kelele, lazima ukumbuke kuomba kibali cha kelele (Noise Permit) uandae na hela ya kibali cha kutumia kelele katika maandamano yako nje ya ile ada ya kuomba kibali cha kuandamana.

Kiufupi ni kwamba kila nchi imeweka utaratibu wake ili kuwasaidia wanaotaka kufanya maandamano ya amani wasiingilie au kuvuruga ratiba za wengine ambao hawana shida na hayo maandamano yako. Sheria na kanuni hizi zinasaidia lengo la maandamano ya amani kutimia kwa amani bila kuvunja sheria za nchi au kuathiri uhuru wa wengine ambao hawana shida na maandamano yako.

Ni vyema ukajua vyema sheria inayosimamia maandamano ya amani iwapo unataka kuandamana kwa amani, pili ni vyema ukazijua vyema adhabu za makosa yatakayotokana na kukiuka sheria na kanuni za kibali cha maandamano ulichopewa.

Yaani kwa mfano umepewa kibali cha kuandamana, sasa ni wajibu wako kuhakikisha kuwa masharti ya kibali hicho yanazingatiwa la sivyo usishangae unafutiwa kibali chako au hata kushtakiwa kwa kukiuka masharti ya kibali cha maandamano yako ya amani.

Mwisho niseme, ni wajibu wa mamlaka husika kujiridhisha na kuamua wakati mzuri wa kukupa kibali husika. Narudia maswali fikirishi. Je, nchi zetu za kiafrika zinatoa vibali vya maandamano ya amani ikiwa makundi au watu katika jamii wanataka kuandamana.

Je, waandamanaji katika nchi zetu za kiafrika wanaheshimu maudhui ya maandamano yanayoitwa ya amani? Je, wanafuata sheria na kanuni zinasosimamia maandamano ya amani?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here