‘Ujerumani ni nchi ya kipumbavu zaidi barani Ulaya’

0

Berlin, UJERUMANI

MBUNGE wa Ujerumani Sahra Wagenknecht ameeleza hivi karibuni kuwa, Serikali ya Taifa hilo ndiyo ya “kipumbavu zaidi” barani Ulaya, kwa kujiingiza katika “vita kamili vya kiuchumi” dhidi ya Russia, ambayo ni msambazaji wake mkuu wa nishati.

Akihutubia bunge la nchi hiyo Bundestag, Wagenknecht, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa zamani wa chama cha mrengo wa kushoto cha Die Linke, amehimiza kukomeshwa vikwazo dhidi ya Russia.

Mwanasiasa huyo wa mrengo wa kushoto nchini Ujerumani, akataka pia makamu wa Kansela na waziri wa uchumi wa nchi hiyo, Robert Habeck ajiuzulu.

Mbunge huyo ameuita mzozo unaoendelea nchini Ukraine kuwa “jinai” na kueleza kwamba, vikwazo dhidi ya Russia ni “janga” kwa Ujerumani yenyewe.

Aidha, ametahadharisha kwa kusema kuwa, kutokana na kukosekana udhibiti wa bei ya nishati, uchumi wa nchi hiyo karibuni hivi “utabaki kama kumbukumbu tu ya siku nzuri za zamani”.

Mwanasiasa huyo machachari, akatoa mwito wa kuondolewa vizuizi na kuanzisha mazungumzo na Russia.

“Kwa kweli tuna Serikali ya “kijinga zaidi barani Ulaya,” aakasisitiza Wagenknecht na kuhoji: “ni ujinga gani huu kudhani kwamba tunamuadhibu Putin, kwa kufukarisha mamilioni ya familia nchini Ujerumani, na kuangamiza sekta yetu ya nishati, huku Gazprom ikijipatia faida ya juu kabisa?”

Ulaya inakabiliwa na hali mbaya ya uhaba wa nishati ambao haujawahi kushuhudiwa, kutokana na kuendelea vita vya Ukraine, na vikwazo vya Marekani na Magharibi dhidi ya Russia, hususan katika sekta ya mafuta na gesi ya nchi hiyo.

Wataalamu wengi wametabiri kwamba, nchi za Ulaya zitakabiliwa na hali ngumu sana wakati wa msimu wa baridi kali, sanjari na kuongezeka matumizi ya nishati katika nchi hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here