WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuifungua wilaya ya Mafia kwa kujenga miundombinu bora ya barabara ili kuchochea fursa za kiuchumi, Utalii na Uwekezaji.
Bashungwa amesema hayo katika mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wananchi wa Kirongwe Wilayani Mafia katika ziara yake ya Kikazi ya kukagua hali ya miundombinu ya barabara pamoja na utendaji wa Kivuko cha MV Kilindoni kinachotoa huduma kati ya Nyamisati – Mafia.
Bashungwa alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa Wizara ya Ujenzi kuanza taratibu za kumpata Mkandarasi atakayejenga barabara ya Kilindoni – Rasmkumbi (KM 52.28) kipande kilichobakia cha Kilometa 50 kwa kiwango cha lami baada ya kukamilisha ujenzi wa kipande cha Kilindoni – Kigamboni (KM 2.1)
“Kwa sababu ya jiografia ya Mafia, barabara ya Kilindoni – Rasmkumbi tukiijenga vipande vipande haitaleta tija na kutakuwa na gharama zaidi kutokana na namna ya kupata vifaa vya majenzi, hivyo ni lazima tulete Mkandarasi mmoja ili akiianza barabara hii abaki huku huku Mafia mpaka barabara hii ikamilike”, alifafanua Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemuelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) mkoa wa Pwani kuikarabati barabara ya kutoka Bungu hadi Nyamisati (KM 40) kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika wakati wa mvua na kiangazi.
“Kwa maboresho tunayoyafanya kwenye kivuko cha MV Kilindoni lazima utoaji huduma wa kivuko uendane na mwasiliano mazuri ya barabara”, alisisitiza Bashungwa.
Hata hivyo, Bashungwa ameahidi kusimamia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kivuko kingine ili kuleta tija kwa wananchi wa Mafia kupata huduma bora za usafiri na usafirishaji.
Naye, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambaye pia nia Mbunge jimbo la Mafia Omary Kipanga ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kukiona Kisiwa cha Mafia na kuleta fedha za miradi mbalimbali, ambazo zimeboresha huduma kwa wananchi wake.