Ufundi stadi umepewa kipaumbele na Serikali – Dkt. Biteko

0

📌 Asisitiza kuwa, Rais Samia anajenga vyuo kila wilaya nchini

📌 Apongeza utoaji wa mafunzo na ujuzi kuendana na teknolojia ya kisasa

📌 Makundi maalumu kupewa kipaumbele

📌 Asema VETA itakuwa msingi kwa malezi ya watoto na Vijana

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuwekeza kwenye ufundi ili Watanzania waweze kujikomboa katika uchumi.

Hayo yamebainishwa leo Machi 21, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya miaka 50 ya utoaji Elimu na Mafunzo ya ufundi Stadi nchini (VETA) iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Biteko alisema kuwa, Serikali imeweka msukumo mkubwa katika ufundi stadi ili Watanzania wapate elimu yenye viwango vikubwa na ujuzi wa kuweza kujikomboa katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anajenga VETA kila wilaya ili kuwapa ujuzi watanzania waweze kuajirika katika sekta zote,” alisisitiza Dkt. Biteko.

Aidha, ameipongeza Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kwa kuwa na maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa hatua hiyo kubwa na kuwataka kuendelea kufanya kazi ili kuwajengea uwezo watanzania katika ujuzi mbalimbali.

“Kwa mara myingine nawapongeza VETA kwa kuendelea kutoa mafunzo na ujuzi kuendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuhakikisha kuwa ujuzi unatolewa kwa kuzingatia ubora na viwango vya kimataifa, ” alisema Dkt. Biteko.

Vile vile, alisisitiza elimu kutolewa kwa watu wenye mahitaji maalumu na wanaotoka kwenye mazingira magumu nchini yaweze kuongeza fursa kwa kila mtanzania kupata elimu ya ujuzi.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda alisema kwamba, Maadhimisho ya Miaka 30 ya VETA ni uhalisia kuwa Serikali imeipa kipaumbele VETA ili vijana wapate elimu ikiwemo kujenga vyuo vya ufundi katika maeneno mengi nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA, Anthony Kasore alisema, VETA imezingatia viwango na ubora wa mafunzo unazingatiwa ili vijana wanaohitimu waweze kumudu soko la ajira.

Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa usimamizi na uwezeshaji wake mkubwa katika mafunzo ya ufundi stadi nchini ili vijana waweze kupata maarifa na ujuzi ya kufanya shughuli za kiuchumi kwa tija.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here