MTENDAJI Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Peter Mwasalyanda, amepokea cheti cha ushiriki katika shindano la Miundombinu ya TEHAMA katika Mkutano wa WSIS +20 uliofanyika jijini Geneva, Uswisi.
Katika mkutano huo, UCSAF iliwasilisha mradi wake wa mawasiliano ya simu Zanzibar, mradi ambao Serikali iliitoa ruzuku ya Shilingi Bilioni 6.9 kwa kampuni ya mawasiliano ya YAS kwa lengo la kufikisha mawasiliano katika shehia 38.
Kupitia mradi huu, jumla ya minara 42 ya mawasiliano ilijengwa katika visiwa vya Pemba na Unguja, hatua ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika eneo hilo.
Kongamano la WSIS+20 limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa kupitia taasisi zake ITU (International Telecommunication Union) na UNCTAD (United Nations Conference on Trade and Development), likilenga kuhamasisha na kuendeleza maendeleo ya teknolojia za mawasiliano duniani.