SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekabidhi vifaa saidizi vya TEHAMA ikiwemo Personal Digital Assistants (PDA), kompyuta na vifaa vingine kwa Shirika la Posta Tanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za mawasiliano na posta nchini.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amesema hatua hiyo inalenga kuifanya Posta kuwa taasisi ya kisasa inayotoa huduma bora, nafuu na jumuishi kwa wananchi wote.

Kwa mujibu wa Waziri, vifaa hivyo vitasaidia kuongeza uwazi, kupunguza ucheleweshaji na kuongeza ufanisi wa Shirika la Posta Tanzania.
Aidha, vifaa hivyo pia vitaboresha kasi ya usambazaji wa barua na vifurushi, sambamba na kufungua milango ya huduma mpya za biashara mtandaoni, malipo ya kidijitali na huduma za Serikali mtandao.

Silaa ameipongeza UCSAF na kusema kuwa, huu ni mfano bora wa mshikamano wa kitaasisi huku akisisitiza kuwa Serikali itabaki thabiti katika kuhakikisha sekta ya Posta na mawasiliano inaendelea kuwa injini ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, sambamba na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali.