TANGU kuanzishwa kwake, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umefanikisha ujenzi wa jumla ya minara ya mawasiliano ya simu 2,250 ambayo imejengwa hadi kufikia Desemba 2025.
Ujenzi wa minara hii ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kupunguza pengo la mawasiliano kati ya maeneo ya mijini na vijijini, kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za simu na intaneti kwa uhakika na hivyo kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali.
Minara hiyo pia inachangia kuboresha huduma za kijamii kama elimu, afya na biashara mtandaoni, huku ikisaidia katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Serikali kupitia UCSAF inaendelea kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano inajengwa pamoja na kuboreshwa kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wote, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini.