UCSAF unavyoyafanya mawasiliano vijijini kuwa rahisi

0

Na Iddy Mkwama

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) unaendelea na utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa minara 758, ambapo hivisasa umefikia asilimia 81.79%.

Mradi huu wenye lengo la kuvifikia vijiji 1407, kata 713 na wilaya zote 127 na mikoa 26 Tanzania Bara, ulisainiwa Mei, 2023 na unatekelezwa na Serikali kwa ushirikiano wa Makampuni ya simu Airtel, Halotel, Honora (YAS), TTCL na Vodacom.

Hadisasa, ili kufikia idadi inayokusudiwa, imebaki minara 138, ambapo mradi huu unalenga kuwafikia wananchi Milioni 8.5 waliopo maeneo ya vijijini na Serikali imetoa ruzuku ya Shilingi Bilioni 126 kwa ajili kuufanikisha.

“Mheshimiwa Rais kwa mapenzi makubwa, aliamua wananchi wote wapate huduma bora za mawasiliano, kwahiyo akaelekeza itengwe ruzuku ya Bilioni 126 kwa ajili ya kuwasaidia watoa huduma kujenga mawasiliano kwenye maeneo ya vijijini,” anasema Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda.

Kupitia mradi huu, Serikali inalenga kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma bora za mawasiliano, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha usawa wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa watanzania wote.

Taarifa kutoka UCSAF zinaonyesha kuwa, hadi kufikia Julai 25, 2025, minara 620 tayari imewashwa na wananchi wanafurahia mawasiliano, huku kasi ya kukamilisha minara iliyobaki ikiendelea ili kuhakikisha kila Mtanzania anaunganishwa Kidigitali.

Kwa miaka ya nyuma kabla ya ujio wa mradi huu, wananchi wa maeneo mbalimbali nchini, walikabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa mawasiliano na wakati mwingine walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maeneo yenye mtandao ili kuwasiliana na ndugu, jamaa na marafiki.

Miongoni mwa waliosahau changamoto hizo ni wananchi wa kijiji cha Endahagichan, Mkoani Manyara ambao wanasema, walipata mawasiliano hafifu tena walilazimika kwenda milimani ili kupata huduma, lakini hivisasa wanapata mawasiliano kwa urahisi.

Wengine ambao wameagana na changamoto za mawasiliano hafifu ni wananchi wa Kijiji cha Engaresero ambao wanasema wanafurahia mawasiliano, tofauti na awali walilazimika kutumia mnara wa nchi jirani ya Kenya na wakati mwingine walikuwa wanatumia minara ya vijiji vya jirani.

Hata hivyo, licha ya kutumia minara hiyo, bado mawasiliano yalipatikana kwa shida, lakini hivisasa baada ya kujengewa mnara kwenye kijiji chao kupitia mradi unaotekelezwa na UCSAF, wanapata mawasiliano ya uhakika popote walipo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Engaresero, anawashukuru na kuwapongeza UCSAF kwa kuwarahisishia mawasiliano, “ukitaka kumtumia mgonjwa hela na yupo hospitalini, unatuma kwa urahisi.”

Simon Zefania, mkazi wa kijiji cha Engaresero anasema, wakati mwingine mawasiliano yao yalikuwa kwa njia ya ana kwa ana, na walikuwa wanawasiliana au kufikishiana ujumbe kwa ndugu zao kwa njia za kizamani; kwa kumpa mtu maagizo kwa mdomo. “Sasahivi mfugaji akiwa machungani unampigia anakupa taarifa anaendeleaje, tukio likitokea ni rahisi kutoa taarifa kwenye vyombo husika.”

Barikiwa Chalanda, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lola, Wilayani Chunya, Mkoani Mbeya anasema, awali kabla ya kujengewa mnara kwenye kijiji chao, walikuwa wanapata mawasiliano hafifu, hivyo walikuwa wanashindwa kutoa taarifa za haraka linapotokea tatizo.

Anasema, kwasasa mbali na kutoa taarifa mbalimbali, wananchi wa kijiji hicho wanapata wepesi wa kuagiza mizigo na ikafika kupitia njia za kisasa za mawasiliano.

“Mawasiliano yatakua kwa kasi, maana unaweza kukaa kwenye kijiji hiki cha Lola, ukamuagizia mtu mzigo kutoka Mbeya na ukafika kwa wakati, nashukuru Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, maana mawasiliano kwa wilaya yetu ya Chunya ilikuwa changamoto kubwa,” anasema Chalanda.

Chalanda alitoa wito kwa UCSAF kuendelea kutatua chagamoto za mawasiliano kwenye maeneo mengine ili kila Mtanzania apate fursa ya kutumia Intaneti.

Kwa upande wa Kata ya Ifwenkenywa ambayo ipo Wilaya ya Songwe, Mkoani Songwe, Afisa Mtendaji Luciano Mwaiteleke, anasema hali ya mawasiliano kwa kata hiyo hususani kwenye eneo kubwa ambalo lina mzunguko mkubwa wa biashara, ilikuwa mbaya.

Anasema, baada ya ujio wa mnara umesaidia kuwakomboa wafanyabiashara na kuwasaidia wananchi ambao wananufaika na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote “Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona namna gani wanatuletea hii minara kwa ajili ya kutatua shida zetu.”

Kwa upande wake Eva Januari, mkazi wa Ifwenkenywa anasema, kijiji chao ni kizuri na kina maendeleo, lakini walikosa maendeleo ya mawasiliano, hivisasa popote alipo hata akiwa chumbani kwake, mawasiliano yanapatikana kwa urahisi.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Winston Ngao, anasema umuhimu wa mawasiliano kwa vijijini ni mkubwa, kwani ndio yanayojenga uchumi, kwasababu kila kitu kinahitaji mawasiliano kwa ajili ya kuokoa muda na kurahisisha mambo.

“Unaweza ukajikuta kwa kitu kidogo tu unatembea kwa miguu umbali mrefu, lakinini sasahivi kutokana na mawasiliano, unamtuma mtu, mambo yanakuwa rahisi sana,” anasema.

Mkazi wa kijiji cha Idete, Kata ya Chanzuru, Mkoani Morogoro, Yahya Chungu anasema, kabla ya kujengewa mnara kwenye kijiji chao, walikuwa wanapitia changamoto mbalimbali wanapotaka kuwasiliana na ndugu zao; walilazimika kupoteza muda mwingi na kuhatarisha usalama wao.

“Ulikuwa unalazimika kwenda sehemu nyingine ambayo kunapatikana mtandao bila kujali usalama wa eneo husika, lakini ilibidi uende ili upate mawasiliano, wakati mwingine ukiwa mbali na nyumbani na unataka kutoa taarifa fulani, ilikuwa inashindikana kutokana na ugumu wa mawasiliano,” anasema.

Anasema, kwasasa baada ya ujenzi wa mnara kwenye kijiji chao, suala la kutafuta mawasiliano na kupoteza muda mwingi na hata kuhatarisha maisha, limebaki historia. “Tunaipongeza Serikali na tupo pamoja na Serikali yetu kuhakikisha tunafurahia mawasiliano yetu.”

Hii ni mifano michache ya baadhi ya vijiji ambavyo tayari wamejengewa minara, vipo vingi na vingine vinaendelea kuboreshewa mawasiliano yao, jambo ambalo linaifanya Tanzania kuwa mfano bora wa kuigwa barani Afrika katika uendelezaji wa huduma za Kidijitali kwa wote.

Mbali na hilo, Tanzania inatajwa kuwa moja ya nchi zenye mafanikio makubwa katika kupeleka huduma za mawasiliano kwenye maeneo ya vijijini, mradi huu ukikamilika, utaiweka nchi kwenye mazingira mazuri zaidi kwenye suala la mawasiliano, kiuchumi na kuchochea maendeleo hususani kwenye maeneo ya vijijini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here