NAIBU Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo Dugange amesema Serikali inatambua umuhimu wa uanzishaji wa Mamlaka mpya za kiutawala ili kuweza kuwafikia Wananchi na kutoa huduma kwa kuzingatia kanuni na sheria za uanzishaji wa Mamlaka hizo.
Alisema, uanzishaji wa maeneo ya utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287, (Mamlaka za Miji) Sura 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014.
Dkt Dugange ameyasema hayo wakati wa akijibu swali Amandus Julius Chinguile Mbunge wa Jimbo la Nachingwea katika kipindi cha maswali na majibu aliyeuliza.
“Je, lini Serikali itapandisha hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo Nachingwea kuwa Halmashauri ya Mji.” katika Bunge la bajeti linaloendelea Jijini Dodoma.
Alisema, mwongozo wa kuanzisha maeneo ya utawala unaanza kwa kusudio kujadiliwa kupitia vikao vya ngazi za Msingi, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea inashauriwa kufuata utaratibu huo na kuwasilisha Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
“Mamlaka nyingi zilizoanzishwa bado zinaupungufu wa miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya utawala na huduma za kijamii, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu katika maeneo ya utawala yaliyopo.” alisisitiza.