Tunajua tatizo linalokwamisha soka letu?

0

Na Yahya Msangi


TATIZO la mafanikio ya timu zetu za soka hususani timu ya Taifa Stars sio kiwanja, sio kocha, wala sio fedha. Rais Mstaafu Hayati Benjamin Mkapa alidhani tatizo la timu yetu ni kiwanja, akawaleta wachina wakajenga kiwanja kizuri.

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akadhani ni kocha, akatuletea Marcio Maximo kutoka Brazil. Rais Hayati Magufuli alidhani tatizo ni fedha, akawaita Ikulu wachezaji wetu akawapa fedha.

Hakika, Rais ambaye unaweza kusema alilijua tatizo la soka letu ni Mzee Mwinyi. Alitambua sisi ni kichwa cha mwendawazimu, akaamua kutopoteza muda wake, akaacha tunyolewe na kila mlevi, lakini kwa kuwa mpaka sasa wapenzi wa soka hatujajua tatizo linaloisumbua timu yetu.

Ukiwasikiliza wadau wengi wa soka kila timu inapofanya vibaya, lawama wanazielekeza kwa kocha, eti hakumpanga fulani au kampanga fulani. Wangependa awapange wanaowataka wao. Moja ya tatizo letu ni kila mtu kujifanya kocha, Maximo yalimshinda, tunao wachambuzi kibao wa soka, lakini nao ukiwasikiliza unapata kinyaa!

Je, soka letu linaugua ugonjwa gani? Tunapaswa tukae chini, tumwangalie mgonjwa vizuri. Tusikimbilie kutoa dawa il-hali hatujaujua ugonjwa. Tutampa mgonjwa wa kipindupindu Klorokwini!
Yapo mambo machache ambayo tunaweza kuyaweka sawa na yakasaidia soka letu.

Nikiwa mpenzi wa soka, Mtanzania na mchezaji wa zamani, kwanza nianze kwa kusema kuwa, enzi za Mwalimu Nyerere tuliwahi kuwa na timu ya Taifa iliyokuwa ikitupa raha kwa kiasi fulani. Kwa hiyo, kama kweli tunamuenzi Mwalimu turudi na kutazama alifanya nini kwenye michezo hadi tukawa tunaogopwa?


Vijana wengi hawajui tuliwahi kuogopwa kwenye soka. Niliwahi kuwepo Cairo kikazi mwaka 2002. Siku moja nikaenda mtaa mmoja wenye maduka karibu na msikiti maarufu wa Al-Azhar. Pale kilipo Chuo Kikuu cha kiislamu. Nilikuwa nimevaa jezi ya Yanga.

Kuna vijana waliponiona tu wakaja wakishangilia! Yanga! Yanga! Yanga! Kumbe ni wa klabu ya Al-Ahly, ghafla wakatokea wengine wakishangilia Simba, Simba, Simba! Kumbe walikuwa ni mashabiki wa Zamalek. Hapo ndio nikajua kumbe hawa ni wapinzani wa jadi.

Kumbe Yanga ikicheza Misri inashangiliwa na Al- Ahly na Simba ikicheza inashangiliwa na Zamalek! Basi tukazungumza sana kuhusu vilabu hivi. Ndipo nikajua historia zao. Kwa hiyo kuna muda tuliwika Afrika.

Je, siri ya enzi ya mwalimu ilikuwa nini? Wakati huo kulikuwa na uongozi mzuri wa vyama vya soka, hakuna jingine! Ni enzi za akina Paul West Gwivaha, Said Ahmad Al- Maamry, Meja Mrisho Sarakikya na wenzao. Hakukuwa na kiwanja cha maana, makocha wa Taifa kutoka nje wala vitita vya fedha kwa wachezaji, lakini tulipata mafanikio.


Ni vyema Wizara husika na Serikali ikajiuliza uongozi mzuri wa vyama vya soka ni upi? Nyerere aliwezaje kuusimika? Ndipo huyu mwendawazimu atapata tiba stahiki. Lakini, tukiendelea kudhani tatizo ni kiwanja, kocha au fedha, basi tujiandae na ugonjwa wa moyo Kitaifa maana Taifa Stars hatapona. Tuache kuwashie lawama makocha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here