TRA yakusanya Trilioni 6.63

0

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 6.63, sawa na ufanisi wa asilimia 95.17 ya lengo la kukusanya Shilingi  Trilioni 6.97 katika kipindi cha robo ya tatu ya Mwaka wa fedha 2023/24.

Mamlaka hiyo imesema, makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 11.68 ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi Trilioni 5.94 ya kipindi kama hicho katika Mwaka wa fedha 2022/23.

Katika taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata alisema katika mwezi Machi 2024, TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 2.49, sawa na ufanisi wa asilimia 97.05 katika lengo la kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 2.56.

Alisema,makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 6.91 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi Trilioni 2.32 kilichokusanywa mwezi kama huo katika mwaka wa fedha 2022/23.

“Makusanyo ya kodi katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha Mwaka wa Fedha 2022/23 Januari tulikusanya Shilingi 2,011,169.93 wakati lengo lilikuwa Shilingi 2.248,412 lakini kwa mwaka huu makusanyo ya Januari ni Shilingi 2,123,332.51 sawa na 94.44%,” alisema.

Aliongeza kuwa:”Februari mwaka huu tulikusanya 2,021,106.00 sawa na 93.70 % wakati lengo lilikuwa ni 2,157,069 hata hivyo, mwaka 2022/23 tulikusanya Shilingi 1,600,841.93.”

Kamishna huyo alisema, mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka ni kuongezeka kwa uhiari wa ulipaji kodi kufuatia maboresho yanayoendelea kufanywa ikiwemo kusogeza huduma jirani na walipakodi.

Alisema, kuanzishwa Divisheni za Walipakodi Wadogo na Walipakodi wa Kati, pamoja na kuendelea kusuluhisha pingamizi za kodi nje ya mahakama zimechangia ukusanyaji huo wa kodi.

Pia, alisema mafanikio hayo yamechagizwa na muitikio mzuri wa walipakodi kuwasilisha kwa wakati ritani za kodi kwa mwaka 2024 kupitia mifumo ya Tehama ya Uwasilishaji wa Ritani.

“Kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji na ukuaji wa shughuli za kiuchumi hapa nchini zinazochangia mapato kama vile sekta za madini, taasisi za kifedha ikiwemo mabenki, sekta ya utalii,” alisisitiza.

Vilevile alisema, kuongezeka kwa ufanisi kwenye huduma za forodha hususani katika kusimamia kodi zinazohusiana na uingizaji wa mizigo toka nje ya nchi.

Akielezea mikakati yao kufikia lengo la ukusanyaji kodi, Kidata amesema wananchi wanapaswa kuendelea kutoa taarifa juu ya vitendo vinayoashiria ukwepaji wa kodi nchini ikiwemo biashara za magendo na uuzwaji wa bidhaa ambazo hazijabandikwa stempu za kielektroniki (ETS).

“Ikumbukwe kuwa kukithiri kwa vitendo hivi haviathiri makusanyo ya mapato ya Serikali pekee, bali vinahatarisha afya na usalama wa wananchi kwa bidhaa hizi kuuzwa sokoni wakati hazina viwango vya ubora kwa matumizi ya binadamu,” alisema.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara wote wanashauriwa kuendelea kutoa risiti za Kielektroniki (EFD) zenye viwango sahihi kila wanapouza bidhaa au kutoa huduma.

“TRA inawashukuru na kuwataka wananchi wote kuendelea kushiriki katika kampeni ya TUWAJIBIKE kwa kudai risiti stahiki za kielektroniki (EFD) zinazobainisha bidhaa na kiasi sahihi kilicholipiwa,” alisema Kidata.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here