TRA imetimiza wajibu na maono ya Rais Dkt. Samia

0
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata.

Mwandishi Wetu

HAIJAPATA kutokea tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka 1996, hadi kufikia Apiril 2024 imekusanya zaidi ya Shilingi Trillioni 21.3. Hii ni asilimia 96.9 ya lengo la mwaka 2023. Ni rekodi inayostahili kila Mtanzania kujivunia, kwani ni dalili njema kwamba, nchi yetu sasa inaelekea kujitegemea.

Kwa mafanikio haya, pongezi ya kwanza ni kwa walipa kodi kwa kuonyesha moyo wa Kizalendo; wamedhihirisha kwa vitendo ule usemi usemao kwamba, Tanzania itajengwa na Mtanzania mwenyewe na haswa kila Mzalendo.

Jitihada zao zimeleta mwanga wa maendeleo, kwa vile kodi wanazolipa zinaimarisha miundombinu ya Kijamii na Kiuchumi ili kukidhi haja na kuendana na kasi ya ongezeko la Watanzania.

Pongezi nyingine ni kwa Serikali ya Rais wa ya Awamu ya Sita, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka Manejimenti ya TRA iliyoweza kutafsiri maono yake kwa kubuni mazingira mapya ya Mamlaka ya Mapato rafiki kwa walipakodi na kuachana na matumizi ya nguvu kukusanya kodi.

Hakika, uteuzi uliofanywa na Rais Dkt. Samia kwa Alphayo Kidatta kuwa Kamishna Mkuu wa TRA, umefanikiwa kukifanya kikapu cha mapato ya Serikali kujaa; Mafanikio haya yameenea kila kona ya nchi, na hilo linaweza kupimwa na jinsi miradi inavyotekelezwa kwa kasi na kwa ufanisi wa hali ya juu.

Aidha, nitakuwa mwizi wa fadhila kuacha kupongeza vitengo mbalimbali vya TRA kwa kazi nzuri ya kutukuka. Pongezi hizi bila shaka zitajenga hamasa na kufanya kazi kwa umahiri zaidi. Ni lazima tukubali kuwa, taasisi hii inalifanya Taifa letu liwe imara. Hakuna asiyejua ustawi wa nchi Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii, unahitaji ulipaji na ukusanyaji kodi.

Menejimenti ya TRA imetufanya Watanzania kutembea vifua mbele kwa kuwa tumeanza kuweka misingi mizuri ya kujitegemea na kusimamia maendeleo yetu. Siku za nyuma wahisani wetu walitumia makusanyo ya kodi zetu za ndani kama silaha ya kutunyima misaada na mikopo. Hivyo, tukawa na nakisi za bajeti.

Chini ya Dkt. Samia tumeshuhudia TRA ikibuni mbinu mbalimbali za kutoa elimu kwa walipakodi ikiwemo kuwashindanisha walipakodi na kuwapatia tuzo na kufanya hivyo, wamewapa moyo wa ushindani na kuondoa ulanguzi na magendo, hivyo mapato yameongezeka.

Mbali na hamasa kwa walipakodi, Menejimenti ya TRA imeleta Mapinduzi makubwa ya TEHAMA kwa kushirikiana na Makampuni yenye uzoefu na kukusanya mapato kwenye bandari na mipaka, hali ambayo imeifanya biashara kukua na kujenga uimara katika udhibiti wa mapato.

Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba aliliambia bunge hivi karibuni kwamba, kuimarika kwa mifumo ya Kielektroniki ya ukusanyaji mapato na kuanza kwa ujenzi mfumo wa usimamizi wa kodi za ndani IDRAS ambao ni mahususi kwa ajili ya usajli, ukadiriaji na ukusanyaji wa kodi na ufutiliaji wa walipa kodi, umesaidia kuleta ufanisi katika mapato ya Serikali.

Kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika, ingekuwa busara kwa wasaidizi wa Rais, kumshauri kuipatia muda zaidi Menejimenti ya TRA ili kuendeleza kazi njema inayofanywa na wazalendo; kuwaondoa Watanzania katika kulipa kodi ridhaa, badala ya mtulinga.

Dkt. Samia ameleta uhuru wa kweli uliomkomboa mwananchi kutoka kwenye minyororo ya ukoloni ulioambatana na kudhalilishwa na kupanua wigo wa walipa kodi ambao sasa wanaona ni fahari kwao kulipa kodi ili mradi Serikali iandae mazingira ya upatikanaji rahisi wa riziki zao za kila siku.

Rekodi ya TRA inatupeleka kwenye nchi ambayo hamasa ya kulipa kodi kwa anayestahili anafanya hivyo. Serikali ina wajibu wa kumfanya mlipa kodi sawa na ng’ombe anayetoa maziwa; anapaswa kulishwa majani ili alete maziwa mengi zaidi. Serikali kupitia bunge wajenge muafaka wa kodi zinazoweza kulipika.

Wakati wa kupitisha Bajeti ya mwaka 2024/25, Wabunge mjini Dodoma walimpongeza Waziri wa fedha, kwa kufanikisha utayarishaji wa bajeti hiyo. Naamini stahili ya kwanza ilipaswa kuwapongeza walipa kodi kwa kutimiza wajibu wao.

Nchi yetu ina walipa kodi wakubwa, wa kati na wadogo, kila kundi kwa ukubwa au udogo wake, wanastahili kupongezwa kwa kuitwa bungeni, kufanya hivyo ni kujenga hamasa na itawafanya waone zaidi thamani yao. Hii ni motisha tosha.

Wananchi kupitia vyama vya siasa na wabunge wao wamekuwa wakidai huduma mbalimbali za Kielimu, Kiuchumi na Kijamii, kudai huko maendeleo kwa lugha nyingine, Wabunge wanaiomba Serikali itoze kodi zaidi ili kukidhi matarajio ya wananchi. Ni vema nguvu hiyo hiyo wanayoitumia kuibana Serikali bungeni, waitumie kuhimiza kila anayestahili kulipa kodi kwa mujibu wa sheria atimize wajibu wake.

Wabunge ndio wanatunga sheria, TRA ni mkono wa Serikali wa kukusanya kodi, wasiishie kushusha lawama kwa wanaojaza kikapu cha nchi. Upo mfano wa Afrika ya Kusini, wamachinga nao wanalipa kodi, hapa kwetu kundi hili kubwa halilipi kodi na wafanyabiashara wakubwa wanawanatumia kuvujisha mapato.

Kongole kwa Dkt.Samia kwenye ukusanyaji mapato, kuna watu wasiopenda haya yanayofanyika, kwani wanataka waendeleze ukwepaji wa kodi, rushwa na magendo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu; hakika hawa si maadui wa Rais tu, bali ni Taifa zima. Wasiruhusiwe wapoteze dira na kutoboa mtumbwi tunaosafiria.

Ukusanyaji kodi ni taaluma, TRA si mahala pa kufanyia majaribio, jitihada na mafanikio makubwa ya ukusanyaji wa mapato ya nchi yanapaswa kuungwa mkono na vyama vya siasa, kwani ujenzi wa nchi yetu utokane na kodi zetu na raslimali zetu, hatuna wajomba.

Ni jukumu la Menejimenti ya TRA kuendeleza nguvukazi ya TRA kwa kuajiri vijana wenye uwezo wa kukusanya mapato ndani ya muda unaotakiwa. Wenye ubunifu wa biashara za Kitaifa na Kimataifa ili kukuza wigo wa walipakodi. Kwa kufanya hivyo, Taifa litaweza kuridhisha kizazi kipya cha walipakodi kwa maendeleo.

“Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni” TRA imetimiza wajibu na maono ya Rais wetu ndani ya kipindi kifupi. Tunapaswa kuisaidia ili kujenga misingi imara ya Taasisi. Ukusanyaji wa Mapato unaofanywa utasaidia ulipaji wa madeni kwa ajili ya miradi ya maendeleo tunayokopa kwenye vyombo vya fedha vya Kimataifa.

Itoshe kusema, Rais Samia ameweza kumfanya mlipakodi au wa ndani na nje ya nchi yetu kuwa na thamani kubwa. Wasaidizi wa Serikali ya Awamu ya Sita wametafsiri vyema sera ya kudhibiti mapato, hamasa ya walipakodi wakubwa na wadogo imekuwa kubwa na tuendako itakuwa fahari kwa Mtanzania kulipa kodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here