Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imeitaka sekta Binafsi Tanzania kutumia fursa ya maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam kuitumia fursa hiyo kufanya biashara na kuongeza mapato ya Taifa kuinua uchumi wa nchi.
Akizungumza wakati wa ziara ya Umoja wa Wafanyabiashara Tanzania (JWT), kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus alisema, maboresho yaliyofanywa yamekidhi vigezo, mahitaji na matarajio ya wafanyabishara na kuiweka bandari kwenye ushindaji wa Kimataifa.
Gallus ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mbossa alisema uwekezaji mkubwa umefanywa kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye miundombinu kama eneo la upakuaji na upakiaji mizigo kwa kutumia vifaa vya kisasa, ambapo kazi hiyo kwa sasa inafanyika ndani ya muda mfupi tofauti na hapo awali.
“Mashine za kupikia na kushusha mizigo yaani ‘Cranes’ zimerahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi mkubwa bandarini hapa. Ni nafasi ya pekee kwa sekta binafsi kuchangamkia,” Gallus alisema.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema TPA ina mpango wa kujenga bandari kavu (ICDs) katika eneo la Shimo la Udongo Kurasini jijini hapa kwa ajili ya kuhifadhia mizigo inayoharibika kwa haraka (perishable goods) kama vile matunda katika vyumba maalum vyenye ubaridi.
“Huko nyuma, mizigo ya bidhaa zinazowahi kuharibika ilikuwa inapitia katika bandari ya nchi jirani, lakini hivi sasa mizigo hiyo itakuwa inahifadhiwa katika bandari kavu ikisubiri kusafirishwa kwenda nje ya nchi,” alisema.
“Kufuatia maboresho tuliyoyafanya, hivi sasa hakuna tena malalamiko ya kuchelewa kutolewa kwa mizigo inayowasili bandarini na badala yake, kutokana na kasi ya utendaji iliyopo, wateja ndio wanaochelewa kuja kuchukua mizigo yao,”
Alisema, TPA ina maeneo makubwa ya kuhifadhi mizigo na kutoa wito kwa wafanyabishara kuchukua mizigo yao kwa wakati bandarini, kwani bandari siyo sehemu ya kuhifadhi mizigo na mizigo yote ya wateja inatakiwa itoke ili kutoa nafasi kwa mizigo mingine.
“Kasi ya ushushaji wa shehena itaboreka zaidi wateja watakapochukua mizigo yao kwa wakati,” alisema Gallus na kuongeza kuwa TPA imejipanga na itaendelea kuwa lango imara la Uchumi.
Naye, Meneja Mahusiano wa Kampuni ya DP World Tanzania, moja ya kampuni iliyowekeza katika bandari hiyo ya Dar es Salaam, Elitunu Mallamia alisema, kinachotokea sasa hivi katika bandari ya Dar es Salaam, ni mizigo kusubiri wateja kuondolewa na siyo uchelewashaji tena kutokana na kasi ya utendaji iliyopo.
“Tumeweza kuhudumia shehena asilimia 25 zaidi kwenye miezi hii ambayo tumefanya kazi kuanzia mwezi Mei 2024 mpaka sasa Januari 2025),” alisema Mellamia na kuongeza kuwa, kwa mwezi Disemba pekee magari 25,251 yalishushwa kwenye meli 16 na kuvunja rekodi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara, Hamis Livembe aliipongeza TPA kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuleta mageuzi makubwa kwenye bandari zote hapa nchini.
“Miaka miwili iliyopita, tulikuwa na kilio cha ucheleweshwaji wa mizigo kutoka bandarini na wakati mwingine biashara zilichelewa kuwafikia wateja kwa wakati,” alisema na kuongeza kuwa, maboresho yaliyofanyika yameleta suluhisho la kudumu.