Na Mwandishi Wetu
KAMISHNA Msaidizi Mwandamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), F. Matembo, ameongoza ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kanda ya Kusini, akilenga kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unakwenda sambamba na malengo ya kitaifa ya uhifadhi na ustawi wa misitu.
Ziara hiyo ya siku mbili ilifanyika kuanzia Juni 7 hadi 8, 2025, ambapo ACC Matembo alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Range Post katika Wilaya ya Namtumbo, iliyopo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Matogoro B.
Pia, alikagua ujenzi wa ofisi katika Shamba la Miti Wino lililoko katika Safu ya Mlima Mgongotema, pamoja na kutathmini maendeleo ya ujenzi wa Shamba jipya la Miti Mpepo.
Akizungumza na wataalamu na viongozi wa miradi hiyo, ACC Matembo aliipongeza Kanda ya Kusini kwa hatua nzuri iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa ukamilishaji wa miradi hiyo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa.
“Fedha zipo za kutosha. Kazi yenu kama wasimamizi ni kuhakikisha miradi yote inakamilika ndani ya mwaka huu wa fedha,” alisema ACC Matembo. “Ni muhimu sana kazi hizi zikamilike kwa ubora ili ziwahudumie Watanzania kwa muda mrefu.”
Aidha, alisisitiza kuwa ufuatiliaji wa karibu na usimamizi makini wa miradi ya miundombinu unapaswa kuwa sehemu ya utendaji wa kila siku kwa lengo la kuhakikisha rasilimali za umma zinaleta tija na kuboresha utendaji kazi wa sekta ya misitu.
Ziara hiyo ni sehemu ya mikakati ya TFS kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakwenda sambamba na malengo ya kitaifa ya uhifadhi, usimamizi endelevu wa misitu, na kuongeza mchango wa sekta ya misitu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Taifa.