Na Mwandishi Wetu, Iringa
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea na juhudi za kulinda na kuendeleza rasilimali za misitu kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji vinavyozunguka Shamba la Miti Sao Hill, lililoko Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Katika kikao kilichofanyika leo, Juni 6, 2025, TFS imekutana na viongozi wa vijiji, madiwani, watendaji na wenyeviti wa vijiji, kikihusisha pia Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri, na maafisa uhifadhi wa TFS. Lengo kuu ni kujadili mikakati ya pamoja ya kulinda misitu dhidi ya uharibifu na uvamizi.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Dkt. Salekwa amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutekeleza mikakati ya uhifadhi kwa kushirikiana na wananchi, huku changamoto zote zinazojitokeza zikishughulikiwa mapema ili kuepusha athari za muda mrefu kwa mazingira.
“Ni muhimu kuhakikisha maeneo ya hifadhi yanabaki salama. TFS, ofisi yangu na viongozi wa vijiji tunapaswa kushirikiana kwa karibu kutoa elimu ya uhifadhi na kulinda vyanzo vya maji pamoja na misitu inayotuzunguka,” alisema Dkt. Salekwa.
Aidha, amekumbusha viongozi wa vijiji kuhusu maeneo yaliyopitiwa na Kamati ya Mawaziri wa Kisekta Nane, ambayo ilibaini uvamizi mkubwa wa misitu na shughuli za kibinadamu kinyume cha sheria.
“Leo nimewaita kuwakumbusha wajibu wenu. Baadhi ya wananchi wamevamia maeneo ya hifadhi, wameweka makazi, kupanda mazao na miti. Haya hayawezi kuvumiliwa. Tunapaswa kuwa wakweli kwa wananchi wetu,” alisema kwa msisitizo.
Dkt. Salekwa amewaagiza viongozi wa vijiji kuhakikisha sheria za uhifadhi zinasimamiwa kikamilifu, kuheshimu mipaka iliyowekwa, na kutoshiriki wala kufumbia macho uvunjifu wa sheria katika maeneo ya hifadhi.
“Zoezi la kuhakiki mipaka linaendelea. Tunahitaji ushirikiano wenu ili tuhakikishe hakuna mtu anayeendelea kuvamia misitu,” aliongeza.
Kwa upande wake, PCO Peter Fitwangile, ambaye alimwakilisha Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, amesema TFS imeendelea kushirikiana na wananchi na viongozi wa vijiji kwa karibu zaidi ili kuimarisha elimu ya uhifadhi wa misitu.
“Tunawahimiza viongozi wa vijiji kushirikiana nasi katika kutatua changamoto kwa wakati. Misitu hii ni chanzo cha mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema Fitwangile.
Naye PCO Said Singano, ambaye ni msaidizi wa Mhifadhi Mkuu upande wa Uendelezaji Msitu, amewataka viongozi hao kuhimiza matumizi salama ya moto hasa katika kipindi hiki cha kiangazi.
“Msimu wa kiangazi unahusisha matumizi mengi ya moto. Tunawaomba viongozi mtoe elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ili kuepuka madhara kama uharibifu wa misitu na vyanzo vya maji,” alisema.
Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za TFS kuimarisha usimamizi shirikishi wa misitu kwa kuzingatia sheria, elimu na ushiriki wa jamii. Wilaya ya Mufindi ni mojawapo ya maeneo muhimu kwa uzalishaji wa miti ya viwandani nchini, hivyo hifadhi thabiti ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.