Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umekabidhi msaada wa madawati 100 yenye thamani ya Shilingi Milioni 8 kwa Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Sokoine, wilayani Mvomero mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa taasisi hiyo kwa jamii.
Msaada huo umetolewa kupitia Shamba la Miti la Mtibwa na kupokelewa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli, ambaye amesema hatua hiyo ni mchango muhimu katika kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi.
“Tunapongeza hatua hii ya TFS kwa kuonesha mfano bora wa uwajibikaji kwa jamii. Tunatoa wito kwa taasisi nyingine kuiga mfano huu ili kwa pamoja tuweze kuboresha sekta ya elimu na huduma nyingine muhimu kwa wananchi,” alisema DC Nguli wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano.
Alitumia nafasi hiyo pia kutoa rai kwa wananchi wa Mvomero kutunza mazingira na rasilimali za misitu kwa kuwa ni sehemu ya urithi wa maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Mtibwa, Abdallah Amir Mchomvu, alisema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya TFS ya kushirikiana na jamii katika maendeleo na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tunatambua changamoto ya uhaba wa madawati kwa shule nyingi. Kwa msaada huu, TFS inadhihirisha kuwa uhifadhi wa misitu unaweza kwenda sambamba na ustawi wa jamii. Tunamshukuru Kamishna wa Uhifadhi Prof. Dosantos Silayo kwa kuidhinisha msaada huu kufika kwa wakati,” alisema Mchomvu.
Wanafunzi wa shule hiyo walionyesha furaha yao baada ya kupokea madawati hayo, wakisema yataboresha mazingira ya kujifunza na kuongeza ufaulu. “Tulikuwa tunasoma kwa zamu, wengine chini au kwa kuchangia dawati moja. Sasa tunaamini tutasoma kwa ufanisi zaidi,” alisema mmoja wao.
Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Sokoine, ambayo imepewa jina hilo kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine, ni miongoni mwa shule kongwe zenye historia ya kipekee katika ukanda huo wa Morogoro.
Hatua hii ya TFS inaelezwa kuwa ni sehemu ya mpango mpana wa taasisi hiyo kushiriki katika miradi ya kijamii kwa kutumia mapato yatokanayo na uvunaji endelevu wa misitu, nyuki, na shughuli nyingine za uhifadhi.