WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kupitia Mradi wa Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya Matishio ya Mabadiliko ya Tabianchi, unaendelea kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha miundombinu rafiki kwa utalii katika maeneo ya hifadhi ya misitu nchini.
Katika Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi, moja ya misitu ya asili ya pekee inayopatikana karibu kabisa na Jiji la Dar es Salaam, mradi huu unajenga jengo la kisasa la mbao kwa ajili ya mapumziko ya watalii.
Jengo hilo, lenye ukubwa wa mita za mraba 72, litakuwa na sehemu tatu za kupumzikia wageni na lina uwezo wa kuhudumia hadi watu 50 kwa wakati mmoja.
Kazi ya ujenzi imefikia asilimia 55 na inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 26, 2025 kwa gharama ya Shilingi Milioni 120.
Kukamilika kwa jengo hili kutakuwa hatua muhimu ya kuboresha huduma kwa wageni na kuongeza mvuto wa utalii wa misitu katika Ukanda wa Pwani.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya kazi, Msimamizi wa Ujenzi, Fredrick Chakyi alisema kuwa mradi sasa unasonga mbele kwa kasi baada ya changamoto za mvua zilizokuwepo awali kupungua.
“Awali mvua zilikuwa changamoto kubwa, lakini hali sasa ni shwari. Tunatarajia kukamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa,” alisema Chakyi.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa Misitu wa Wilaya ya Kisarawe, Baraka Mtewa, alieleza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati mpana wa TFS wa kuimarisha utalii wa misitu na kuhifadhi bioanuwai kwa njia endelevu.
“Mradi huu utasaidia kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi, kuongeza mapato ya hifadhi, na kuchochea maendeleo ya kijamii kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka Msitu wa Pugu Kazimzumbwi,” alisema Mtewa.
Kwa msaada wa UNDP na ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF), mradi huu unalenga kulinda mazingira ya asili, kuimarisha uthibiti wa mabadiliko ya tabianchi, na kukuza ushirikiano kati ya Serikali, jamii, na wadau wa maendeleo.