HALMASHAURI ya Manispaa ya Temeke chini ya Mkurugenzi wake Jomaary Satura na Mstahiki Meya Uzairu Athuman jana Januari 30, 2026 imesaini Mkataba wa Ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Mji Mpya na Kampuni ya Ramada Construction Engineering Company pamoja na Kampuni ya Kinjekitile General Trading Company LTD.
Akizungumza kabla ya Utiaji saini wa Mkataba huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Jomaary Satura amesema kuwa Jengo hilo litakua na Vyumba 53 pamoja na Viwanja vya Michezo ambalo litagharimu Shilingi Bilioni 6.9 fedha ambazo zimetokana na Makusanyo ya Mapato ya ndani ya Manispaa ya Temeke.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Uzairu Abdul Athuman ameyataka Makampuni hayo ya Ujenzi kuhakikisha kuwa wanatekeleza zoezi la Ujenzi kwa wakati na kuhakikisha kuwa Ujenzi unaendana na thamani ya fedha zilizotolewa.
“Ujenzi lazima uendane na kasi tunayoitarajia, tunatarajia kuiona thamani ya fedha hii kwenye Ujenzi, Serikali itafika mpaka kwenye maeneo ya Ujenzi kuona mnaendeleaje,” alisema Uzairu Abdul.
Aidha, Mstahiki Meya ametoa rai kwa Wananchi kuendelea kuiamini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwaomba Wananchi waendelee kulipa kodi ili kuiwezesha Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kupiga hatua katika maendeleo.
