Teknolojia ya kuondoa uvimbe mwilini bila upasuaji yazinduliwa

0

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amezindua teknolojia ya kuondoa uvimbe mwilini bila upasuaji inayofahamika kama High-Intensity Focused Ultrasound (HIFU) katika Hospitali ya Kairuki ikiwa ni mara ya kwanza kwa huduma hiyo kuzinduliwa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Akizindua huduma hiyo Agosti 27, 2025 jijini Dar es Salaam, Dkt. Biteko amepongeza Watendaji wa hospitali ya Kairuki pamoja na muasisi wake Hubert Kairuki na Mkewe kwa uthubutu wao katika masuala mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma hiyo ya HIFU ambayo imeiweka Tanzania katika rekodi ya kutoa uvimbe bila kufanya upasuaji barani Afrika suala ambalo pia litaongezea nchi mapato.

Ameeleza kuwa awali huduma ya HIFU barani Afrika likuwa ikipatikana katika nchi tatu tu ambazo ni Misri, Nigeria na Afrika Kusini.

Aidha, ameipongeza Hospitali ya Kairuki kwa kutoa punguzo la asilimia 50 la gharama za matibabu ya utoaji uvimbe bila upasuaji kwa wagonjwa 50 wa kwanza ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo ikiwa ni kielelezo cha Watendaji wa hospitali hiyo kuonesha utu kwa Watanzania, kuacha alama njema na kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kutoa huduma kwa watanzania kwa gharama nafuu.

Dkt. Biteko alisema, kufanyika kwa tukio hilo muhimu ni kielelezo cha Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipa msukumo sekta binafsi na kuikuza ili kutoa huduma za matibabu kwa wananchi kwa ufanisi na kusogeza karibu huduma ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani ndani ya nchi hivyo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono Sekta binafsi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here