Na Mwandishi Wetu
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda, ametaja matumizi ya teknolojia kama moja ya njia zitakazotumika kuwabaini wafanyabiashara mitandaoni wataokwepa kodi.
TRA kupitia kwa Kamishna huyo, mapema Julai 24, walitangaza kuanza zoezi la usajili kwa wafanyabiashara wanaouza na kutangaza bidhaa zao mitandaoni, ambapo waliwataka hadi kufikia Agosti 31 wawe wamejisajili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Agosti 9, 2025 kwenye semina iliyowahusisha TRA na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, kampuni za simu na Wahariri wa vyombo vya habari, iliyofanyika kwenye Hoteli ya Serena alisema, kama ambavyo biashara zinavyofanyika mitandaoni, nao watawafuata wafanyabiashara huko huko.

“Nyie mnauza ‘online’ nasisi tutawafuata online, tutatumia teknolojia,” alisema na kuongeza kuwa, watawabaini hata wale ambao watafanya mauzo kwa fedha taslimu.
Mwenda alisema, mbali na njia hiyo, watatangaza dau kwa watakaotoa taarifa kwa wafanyabiashara ambao wanakwepa kodi, ambapo anayetoa taarifa hizo na kodi ikilipwa, mtoa taarifa atalipwa asilimia 3%.
Alisema, watahakikisha wanarahisisha utoaji wa fedha hizo za zawadi; “kwa mbinu hii hatuwezi kushindwa kutapata taarifa, tutapata tu, tutatumia teknolojia kufuatulia, lakini tutatumia wazalendo.”

Aidha, Kamishna Mwenda alisema, tayari amewaagiza wasaidizi wake kuhakikisha wanawaita wafanyabiashara wote wa mitandaoni ili wazungumze kama kuna changamoto wanazokabiliana nazo.
Alisema, lengo la TRA ni kutaka kutengeneza utaratibu mzuri wa ukusanyaji mapato kwa wafanyabiashara wa mtandaoni ambao utavutia na utakuwa rahisi kuanzia kwenye kujisajili na hata kwenye malipo.
Katika hatua nyingine, Kamishna Mwenda alisema pamoja na maombi ya wadau waliotaka muda wa kujisajili uongezwe, suala hilo halitowezekana kwa wafanyabiashara wakubwa wanaofanya biashara ya nyumba za kupangisha, lakini watafanya hivyo kwa wafanyabiashara wadogo.

Alisema, sababu za kuongeza muda kwa wafanyabiashara wadogo ni ili watoe elimu zaidi na kuwajua zaidi “hawa wanaofanya biashara za u-winga tutawaongezea muda, ila tutakaa nao, lengo ni kuwawezesha, muwe na amani,”
Kamishna huyo wa TRA alisema, moja ya faida watakazopata wafanyabiashara watakaojisajili na kuachangia kiasi kidogo cha fedha, ni kuepuka usumbufu wa kudaiwa kodi kubwa, pia watakopesheka kwasababu kutakuwa na taarifa zao kwenye mfumo.
“Ukifanya janja janja, ukikamatwa na watu ambao sio waaminifu, watakutoza kodi kubwa, itakuletea ‘stress,’ nataka tuzungumze, tuwawezeshe mfanye biashara zenu kwa amani,” alisisitiza Kamishna Mwenda.
