Tanzania yashinda Tuzo 27 kati ya 60 za utalii Duniani

0

TANZANIA imeandika historia mpya baada ya kushinda jumla ya Tuzo 27 kati ya Tuzo 60 zilizotolewa kwenye Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards – WTA), zilizofanyika nchini kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.

Katika ushindi huo wa kihistoria, upande wa Serikali umenyakua Tuzo 11 zikiwemo za vivutio bora vya utalii, Bodi bora ya Utalii Afrika, Nchi bora ya Utalii wa Safari Afrika pamoja na Uwanja wa Ndege bora Afrika.

Kwa upande wa sekta binafsi, kampuni mbalimbali za utalii, hoteli na huduma za kitalii zimefanikiwa kutwaa Tuzo 16. Hizi ni pamoja na Kampuni bora za Utalii wa Safari, hoteli zenye huduma bora, pamoja na hoteli zenye fukwe bora zinazovutia watalii kutoka kona zote za dunia.

Mafanikio hayo makubwa yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia hatua mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa filamu ya Royal Tour iliyotangaza vivutio vya nchi kimataifa, kuongeza bajeti ya sekta ya utalii, kuboresha miundombinu kwenye maeneo ya hifadhi na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji.

Ushindi huo umeonesha wazi Tanzania imejipambanua kama kitovu cha utalii barani Afrika na duniani, ikiwa na dhamira ya kuendeleza utalii endelevu utakaowanufaisha wananchi na kukuza Pato la Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here