Na Mwandishi Wetu, Dubai
TANZANIA imeongoza kikao cha Kamati Namba 4 katika Mkutano Mkuu wa 28 wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) inayoendelea jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ikiwa ni sehemu ya majukumu yake kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambayo Mwenyekiti wake ni Ujerumani.
Katika kikao hicho, Tanzania iliwakilishwa na Constantine Kasese kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), huku Ujerumani ikiwakilishwa na Felix Blaich.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa na kamati hiyo ni pamoja na Mpango wa Huduma na Bidhaa za Posta kwa mwaka 2026–2029, Mfumo wa Ulipaji wa Huduma za Posta kwa mwaka 2026–2029, na Mpango wa Ubora wa Huduma za Posta kwa mwaka 2026–2029
Aidha, Kamati Namba 4 pia itajadili na kuridhia kanuni zitakazotumika katika kuendesha biashara za posta kimataifa kwa kipindi cha 2026–2029, sambamba na kupitisha mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ya UPU kwa kipindi hicho.
Mkutano Mkuu wa 28 wa Umoja wa Posta Duniani umeendelea jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu ikiwa ni siku ya tatu tangu kufunguliwa rasmi Septemba 8, 2025.