Tanzania yachukua hatua kusimamia maeneo ya bahari yaliyohifadhiwa

0

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amesema Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti za kusimamia maeneo ya bahari yaliyohifadhiwa.

Alisema, hatua hizo zimesaidia kukuza usimamizi endelevu wa uvuvi na kuongeza uwezo wa kuzuia uchafuzi wa baharini na kukabiliana na hatari za mabadiliko ya tabianchi.

Mhandisi Masauni alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Kamati Tendaji ya Mkataba wa Nairobi kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi Baada ya Mkutano Mkuu wa 11 wa nchi Wanachama uliofanyika jijini Dar es Salaam, Januari 30, 2025.

Alieleza kuwa, eneo la Bahari ya Hindi Ukanda wa Magharibi lina mifumo mbalimbali ya ikolojia ya pwani na baharini ambayo inasaidia uchumi wa ndani na kitaifa hivyo ni muhimu kuwa na usimamizi endelevu wa mazingira yake.

Masauni alitaja ukanda huo kutoa huduma muhimu za mfumo ikolojia ikiwemo ni makazi kwa bioanuai ya baharini na inachukuliwa kuwa moja ya mifumo ikolojia yenye thamani zaidi ulimwenguni ambayo ina manufaa makubwa kwa jamii za pwani.

Aidha, alishukuru na kupongeza Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira kupitia Sekretarieti ya Mikutano ya Nairobi kwa kusimamia ajenda ya mazingira kupitia ufadhili wa miradi yenye lengo la kuboresha maisha ya jamii za wavuvi katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Tanzania.

Halikadhalika, alitoa shukrani kwa Umoja wa Mataifa kwa kuipatia Serikali takriban dola 70,000 kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kutibu Majitaka cha Msingini, Chake Chake, Pemba.

Masauni aliongeza kuwa, eneo la Pwani ya Tanzania lina rasilimali nyingi za baharini ambazo ni pamoja na fukwe za mchanga, miamba, mito mikubwa ya mito, misitu ya mikoko, nyasi pana za bahari, miamba ya matumbawe na tambarare zenye matope.

Sanjari na hilo, Masauni alisema mazingira ya bahari katika eneo la Tanzania yanasaidia upatikanaji na ukuaji wa aina mbalimbali za samaki kama vile papa, miale, kasa, matumbawe, nyasi za baharini na mikoko ambayo inasaidia katika utunzaji wa mazingira.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here